Jumamosi, 27 Julai 2024

JAJI MFAWIDHI SONGEA AIPONGEZA OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI

Na Mwandishi Wetu-Mahakama, Songea

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha imeipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano na utendaji kazi mzuri kwa kuhakikisha kuwa kesi zote zinaendeshwa vizuri kwa kufuata sera ya Mahakama ya kufanya Usuluhishi katika mashauri ambayo yanaweza kuisha kwa njia hiyo mkoani Ruvuma.

Akizungumza na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo alipofika Ofisini kwake Mahakama Kuu mjini Songea wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Songea na kuangalia mahusiano baina ya Ofisi hiyo na wadau wake mbalimbali ikiwemo Mahakama, Mhe. Karayemaha alisema Ofisi hiyo imekuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha mashauri yanaendeshwa kwa ufasaha na kwa wakati bila shaka lolote.

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Songea inashirikiana na Mahakama kutoa elimu ya sheria kwa jamii kupitia Redio na mabanda ya maonesho na wakati wote Mawakili wa Ofisi hii wanafika mahakamani kwa wakati na kutoa huduma inayostahiki,” alisema Jaji Karayemaha.

Kwa upande wake Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano wanaowapatia Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mkoani Songea na kupelekea kutekeleza majukumu yao kwa amani, weledi na ufanisi mkubwa.

Bi. Mtulo alitoa rai kwa watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Songea kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi kwa maslahi mapana ya Taifa na kwa ustawi utawala wa sheria.

Pia, Bi. Mtulo alionana na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, ndugu Joel Mbewa na kumshukuru kwa ushirikiano na kuiongezea Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Songea vyumba vya Ofisi ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Mtulo, Wakili wa Serikali Mfawidhi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mkoani Songea, Bw. Egidy Mkolwe alisema, Ofisi ya Wakili Mkuu imeendelea kuiwakilisha Serikali mahakamani na katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika mashauri yote yanayofunguliwa na wananchi dhidi ya Serikali katika mkoa huo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo (hayupo pichani) ya kukagua utendaji kazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Songea tarehe 25 Julai, 2024.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Elizabeth Nyembele akizungumza wakati Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo (hayupo pichani) alipofika Ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Songea

Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo akisaini kitabu cha wageni alipofika Ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Songea

Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Egidy Mkolwe akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo (hayupo pichani) alipofika Ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (hayupo pichani) wakati wa ziara hiyo.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)






 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni