Jumapili, 28 Julai 2024

JAJI NDUNGURU ATETA NA WATUMISHI WA MAHAKAMA KUU IRINGA

Na LUSAKO MWANG’ONDA, Mahakama-Iringa

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa wamesisitizwa kufanya kazi kwa umakini muda wote kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanaridhishwa na huduma mbalimbali zitolewazo na Mahakama. 

Akizungumza na Watumishi wa Kanda hiyo kwa mara ya kwanza tangu ahamie hapo hivi karibuni, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru aliwasisitiza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na umaridadi kwa kila mfanyakazi, utunzaji wa mazingira, umuhimu wa kijiendeleza kitaaluma, utunzaji wa mazingira na umuhimu wa mazoezi kwa ajli ya kutunza afya.

“Ofisi yangu ipo wazi kwa ajili ya mtumishi yoyote kufika na kutoa mawazo yoyote ambayo atakuwa nayo ili kushauri juu ya kitu chochote ili mradi kiwe ni kwa maana ya kujenga huku akisisitiza kuwa ofisi yake haitakuwa tayari kumpokea mtu yeyote atakayekuwa anakwenda kupeleka maneno ya majungu,” alieleza Jaji Ndunguru. 

Aliongeza kwa kusema kuwa, “mimi siyo muumini wa majungumajungu, ukiona jambo unalotaka kulileta kwangu ni kwa ajili ya kupika majungu juu ya mtu mwingine ni bora usije maana siko tayari kusikiliza majungu.” 

Jaji Ndunguru amehamia Mahakama Kuu Kanda ya Iringa akitokea Mahakama Kuu Mbeya, amechukua nafasi ya Mhe. Ilvin Mugeta ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa Mhe. Dunstan Ndunguru (katikati) akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa Kanda hiyo hivi karibuni (hawapo katika picha). Kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Angaza Mwipopo na kulia kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Saidi Kalunde.
Sehemu ya Watumishi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa wakimsikiliza Jaji Mfawidhi, Mhe. Ndunguru (hayupo katika picha) alipofanya kikao na watumishi hayo hivi karibuni.
Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Doris Kisanga (aliyesimama) akisisitiza jambo  kwa watumishi (hawapo katika picha) wakati wa kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni