Jumapili, 28 Julai 2024

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA AFURAHIA MAFUNZO YA NDANI NA VIKAO VYA WATUMISHI ARUSHA

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama Kuu Arusha

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amefurahishwa na utaratibu wa Mahakama Kanda ya Arusha wa kufanya mafunzo ya ndani na vikao vya watumishi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi. 

Prof. Ole Gabriel aliyasema hayo tarehe 26 Julai, 2024 alipowasalimia watumishi wa Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) jijini Arusha ambapo pia aliwahimiza Watumishi hao kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na maarifa ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kuendelea kuwa kinara wa kutoa huduma bora kwa wananchi.

 “Nimefurahishwa na utaratibu wa kufanya mafunzo, hata hivyo Mahakama inaendelea kulipia masomo ya watumishi kwa lengo la kuwajengea uwezo na maarifa ya kufanya kazi na hatimae Mahakama kuweza kutoa huduma bora,” alisema Prof. Mtendaji Mkuu.

Aliwahimiza watumishi kutumia fursa ya uwepo wa vyuo mbalimbali mkoani Arusha kujiendeleza kitaaluma kwa faida yao wenyewe na Mahakama.

Kadhalika, Prof. Ole Gabriel alitoa ufafanuzi wakati akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na watumishi ikiwemo maslahi ya watumishi ambapo aliwasisitiza watumishi kujijengea utamaduni wa kuwa na nidhamu ya fedha na kuishi kwa kadri ya viwango vya mishahara yao ikiwa ni pamoja na kuepuka tamaa zisizo na msingi.

Aliongeza kuwa, Uongozi wa Mahakama ya Tanzania unaendelea kufanya juhudi za kila namna kuhakikisha kuwa maslahi ya watumishi wake yanaboreshwa kadri inavyowezekana. 

Aidha, katika kikao darasa hicho, watumishi wa Kituo hicho walipatiwa mafunzo juu ya umuhimu wa kuwekeza kiuchumi katika Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT AMIS), Mafunzo ya kuomba mikopo (e-Loan) na likizo (e-Leave) katika Mfumo wa Kielektroniki wa Utumishi (ESS).

Mada juu ya namna mbalimbali mtumishi anaweza kuwekeza katika Mfuko wa Pamoja wa Uwekezaji na faida zinazopatikana ilitolewa na Afisa ktoka Mfuko huo Mkoa wa Arusha, Bi. Victoria Burra, Mada ya uombaji mikopo kielektroniki ilitolewa na Afisa wa Benki ya CRDB Mkoa wa Arusha, Bi. Vaileth Mlimbo na mada ya uombaji likizo kimtandao ilitolewa na Afisa Tawala Mwandamizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Bw. Seth Kazimoto.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Nyigulile Mwaseba, Jaji wa Mahakama KuuKanda ya Arusha, Mhe. Dkt. Dafina Ndumbaro, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya na Hakimu Mkazi  Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mhe. Erasto Philly.  


Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto) na Viongozi wa Kituo hicho. Wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Dkt. Dafina Ndumbaro, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Amir Msumi na wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha, Bw. Festo Chonya. Mtendaji Mkuu alipita Kituoni hapo tarehe 26 Julai, 2024 kwa lengo la kusalimia watumishi.
Afisa wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT AMIS), Bi. Victoria Burra akiwasilisha mada juu ya namna mbalimbali za kuwekeza katika mfuko huo. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 26 Julai, 2024.

Afisa wa Benki kutoka CRDB, Bi. Vaileth Mlimbo akiwasilisha mada juu ya kuomba mkopo (e-Loan) katika mfumo wa Kielektroniki wa Utumishi (ESS). Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 26 Julai, 2024.

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Arusha wakipatiwa mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 26 Julai, 2024.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni