Jumanne, 9 Julai 2024

MSAJILI MKUU AFANYA ZIARA YA KUSTUKIZA MAHAKAMA LUSHOTO, KOROGWE

Na Mwandishi Wetu-Mahakama

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya jana tarehe 08 Julai, 2024 alifanya ziara ya kushtukiza katika Masjala za Mahakama ya Wilaya Lushoto na Korogwe na kujionea namna watumishi wanavyofanya kazi.  

Mhe. Nkya alipokelewa na kutembezwa kwenye Masjala na Ofisi za Mahakama ya Wilaya ya Lushoto na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka.  Kwa upande wa Mahakama ya Wilaya Korogwe, alipokelewa na kutembezwa na Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe Flora Fredie Bhalijuye.

Wakati wa majadiliano na watumishi, Msajili Mkuu alipokea taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hizo na kuwahimiza kutekeleza mambo kadhaa, ikiwemo kutumia ipasavyo mfumo wa uratibu na usimamizi wa mashauri yaani, e-CMS, kupokea, kusajili na kusikiliza mashauri kupita mfumo.

Mhe. Nkya alihimiza Mahakama za Mwanzo kutumia ipasavyo mfumo wa kuratibu mashauri uitwao Primary Court App, akawataka watumishi wanaohudumu kwenye vioski kutokutumia akaunti zao za mfumo wa kuratibu mashauri. 

Alisema kuwa wakati wa kuwahudumia wadaawa kupitia vioski wahakikishe wanatumia akaunti za wadaawa na namba zao za simu na siyo vinginevyo.

Kadhalika, Msajili Mkuu alihimiza kutokuwa na mlundikano wa mashauri na Mahakimu kujiwekea malengo la kumaliza mashauri ndani ya miezi mitatu kwa Mahakama za Mwanzo na mwaka mmoja kwa upande wa Mahakama za Wilaya.

Mhe. Nkya aliwataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidiii na ushirikiano na kuahidi, kwa kushirikiana na Viongozi wa Mahakama, kuendelea kuboresha miundombinu ya Mahakama ili kuwa na mazingira bora na wezeshi ya utoaji haki nchini.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni