Jumatatu, 8 Julai 2024

MAJAJI WAWILI DIVISHENI YA ARDHI WATEMBELEA BANDA LA MAHAKAMA SABASABA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Majaji wawili kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Arafa Mpinga Msafiri na Mhe. Dkt. Theodora Nemboyao Mwenegoha leo tarehe 8 Julai, 2024 wameungana na Watanzania wengine kutembelea Banda la Mahakama ya Tanzania lililopo kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa 2024, maarufu Sabasaba.

Majaji hao waliwasili katika Viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke katika Mkoa wa Dar es Salaam majira ya saa 9.30 alasiri na kupokelewa na Viongozi wa Mahakama na baadaye kutembelea Banda hilo ambalo limesheheni Wataalam wa masuala mbalimbali ya kisheria kutoka Mahakama ya Tanzania na Wadau.

Wakiwa katika Banda hilo, Majaji hao wamejionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali, ikiwemo maendeleo katika miundombinu ya majengo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo yanalenga kurahisisha na kuharakisha jukumu la utoaji haki kwa wananchi.

Mahakama ya Tanzania imeweka kambi katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’, 2024 yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa huduma na elimu kwenye masuala mbalimbali ya Mahakama na sheria kwa ujumla.

Kwa mwaka huu, Viongozi na watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau mbalimbali ambao ni watalaam na wabobezi katika masuala ya kisheria wanaendelea kutoa huduma na elimu hiyo kwa muda wote wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’ ambayo yameanza tangu tarehe 28 Juni, 2024.

Katika kipindi chote cha Maonesho hayo, Mahakama inatoa huduma mbalimbali zikiwemo za kusikiliza Mashauri kwenye Mahakama Inayotembea ‘Mobile Court Services’, kutoa Msaada wa Kisheria ‘TLS’, elimu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani na safari ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi na Maonesho Mahakama, Mhe. Hussein Mushi, ametoa rai kwa wananchi kutumia nafasi adhimu inayotolewa na Mahakama kwa kuwaleta pamoja watumishi wake na wadau katika kutoa elimu ya sheria bure na kuelimisha taratibu mbalimbali za kupata haki mahakamani.

“Nawaomba wananchi kutumia fursa hii ya maonesho kuja kutoa maoni, malalamiko pamoja na kupata msaada wa kisheria kutoka kwa Mawakili-TLS, Kituo cha Haki na Msaada wa Kisheria pia kujua taratibu mbalimbali za kimahakama,” amesema Mhe. Mushi.

Mhe. Arafa Mpinga Msafiri (wa kwanza kushoto waliosimama kulia) na Mhe. Dkt. Theodora Nemboyao Mwenegoha (katikati) wakipata maelezo katika Banda Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri, wa kwanza kulia ni Afisa Utumishi, Bi. Gaudencia Bruno. Picha chini wakiwa katika Banda la Idara ya Kumbukumbu na Huduma za Maktaba.


Mhe. Arafa Mpinga Msafiri (kushoto) na Mhe. Dkt. Theodora Nemboyao Mwenegoha wakiwa katika Banda la Divisheni ya Ardhi. Picha chini wakiwa katika Banda la Tume ya Utumishi wa Mahakama.

\

Mhe. Arafa Mpinga Msafiri (kulia) na Mhe. Dkt. Theodora Nemboyao Mwenegoha wakiwa katika Banda la Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA). Picha chini wakiwa katika Banda la Kurugenzi ya Ukaguzi, Usimamizi wa Huduma za Mahakama na Maadili.


Mhe. Arafa Mpinga Msafiri (kulia) na Mhe. Dkt. Theodora Nemboyao Mwenegoha wakiwa katika Banda la Mahakama ya Afrika Mashariki. Picha chini wakiwa ndani ya Mahakama Inayotembea.

Picha na Jeremia Lubango.


 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni