Jumatano, 3 Julai 2024

WATUMISHI KITUO JUMUISHI KINONDONI WAPATIWA MAFUNZO

Na Tumaini Shita-Mahakama, Kinondoni

Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni hivi karibuni walipatiwa mafunzo ya siku moja kuwajengea uelewa katika kutokomeza unyanyasi na ukatili wa kijinsia kwa watoto na makundi maalum, kama wazee na walemavu. 

Akitoa mada kwenye mafunzo hao, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni katika Kituo hicho, Mhe. Is-Haq Kuppa alisema suala la ukatili ni la kila mmoja na kabla halijafika katika hatua ya kusikilizwa mahakamani hupitia mchakato katika sehemu mbalimbali. 

Mhe. Kuppa alizitaja sehemu hizo kama mapokezi, masijala na kwa wadau wengine waliopo kituoni hapo kama vile ofisi ya Taifa ya Mashtakaustawi wa jamii, polisi na magereza. 

Alisisitizwa kwamba wahusika wote hao wanalo jukumu la kuwatendea manusura matendo ambayo hayatakuwa sehemu ya kuwaongezea machungu waliyopitia.

Kwa upande wa usikilizaji mashauri, Mahakimu wamekumbushwa kuangalia namna bora ya kushughulikia uendeshaji wa shauri la mtoto, ikiwemo uwepo wa lazima wa afisa ustawi na namna ya muundo wa ukaaji wakati wa kusikiliza mashauri hayo, kama sheria ya mtoto, kanuni na miongozo mbalimbali iliyopo. 

Imesisitizwa pia kwa upande wa makundi maalum umuhimu wa kuendesha mashauri yao bila hisia au dhana mbaya kwa waliyopitia mara baada ya ushahidi wao kutolewa, pamoja na kuhakikisha wanapokuja mahakamani ushahidi wao upokelewe bila kuahirisha bila sababu za msingi. 

Mhe. Kuppa alibainisha kwamba kufanya hivyo itakuwa ni kutenda haki kwa kila upande na kwa tahadhari kubwa kwa makundi hayo kwa kuwa tayari wanakuja mahakamani wakiwa wamepitia madhila makubwa. 

Mafunzo hayo yalihusisha watumishi wa kada zote kutoka Mahakama ya mwanzo Kinondoni,Mahakama ya Wilaya Kinondoni na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni