Alhamisi, 1 Agosti 2024

JAJI MKUU AONGOZA KIKAO CHA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA

 ·       Katibu Apongezwa kwa Usimamizi Mzuri wa Rasilimali  

·        Sekretarieti ya Tume na Mahakama ya Tanzania wapongezwa kwa kazi nzuri.

Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameongoza kikao cha kawaida cha Tume ambacho pia kimempongeza Katibu wake Prof. Elisante Ole Gabriel kwa usimamizi mzuri wa rasilimali uliopelekea Tume kupata hati safi ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Aidha, kikao hicho cha Tume pia kimeipongeza Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama ya Tanzania kwa kazi nzuri iliyofanyika katika kipindi hicho.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika jana tarehe 31 Julai, 2024 jijini Dar es salaam, Katibu wa Tume na Mtendaji Mkuu wa Mahakama alisema kikao hicho pia kilijadili taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama (Fungu 12) na Mahakama (Fungu 40) kwa kipindi cha Mwaka wa fedha uliomalizika wa 2023/2024.

Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya Tume, Prof. Ole Gabriel alisema katika kipindi hicho, Tume ilimshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu uteuzi wa Majaji 24 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Msajili Mkuu wa Mahakama, Msajili wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu. Pia, katika kuimarisha utendaji wa Mahakama, Tume ilimteua Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Naibu Wasajili 30 Katibu wa Jaji Mkuu na kuwathibitisha katika cheo Viongozi 49 baada ya kumudu vema majukumu yao.

Alisema Tume pia iliwathibitisha kazini watumishi 207 na kupandisha vyeo watumishi 2,361 wa kada mbalimbali pamoja na kwabadilisha Kada watumisih 124 waliopata sifa. Aidha, katika kipindi hicho Tume iliajiri watumishi wa Mahakama 112 katika kada mbalimbali.

Kuhusu Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama, alisema katika kikao hicho, Tume ilipokea taarifa kuwa katika kuimarisha utendaji wa Kamati hizo,  Mafunzo ya Uratibu na Usimamizi wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kuhusu uendeshaji wa Mashauri ya Maadili na Nidhamu yalifanyika katika Mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Mwanza, Mara, Manyara na Arusha yakiwa na lengo la kuzijengea uwezo Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kuhusu njia bora ya kushughulikia mashauri ya nidhamu yanayowasilishwa kwenye vituo vyao.

 

Alisema, waliojengewa uwezo walikuwa ni Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya na Mawakili wa Serikali.

 

Aidha, Katibu wa Tume alisema kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika utekelezaji wa bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/24, maeneo yaliyopewa kipaumbele ni uharakishaji utatuzi wa mashauri ya kawaida na mkakati wa kumaliza   mashauri ya muda mrefu (Backlog),kuboresha mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kama nyenzo muhimu ya kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha uwezo katika ukaguzi na usimamizi wa shughuli za Mahakama;

Aliyataja maeneo mengine kuwa ni kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu, ikiwa ni pamoja na mafunzo, na nidhamu ya watumishi, kuongeza ushirikiano na wadau wa haki jinai ili kuharakisha huduma ya utoaji haki; kuendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali.

”Kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali nchini, kumesogeza kusogeza huduma za Mahakama karibu na Wananchi na kuwapunguzia wananchi gharama ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya Haki”, alisema.

Prof. Ole Gabriel alisema kusimika Mfumo wa akili bandia wa transcription and translation solution wa mashauri katika vituo 11 vya Mahakama Kuu, pia ni mafanikio makubwa ndani ya Mhimili wa Mahakama.

 

Aliyataja mafanikio mengine kuwa ni maboresho ya Matumizi ya TEHAMA katika  huduma zinazotolewa na Mahakama mfano: Kukamilika na kuanza kutumika Mfumo mpya wa usimamizi wa mashauri na kuendelea kufanya udhibiti na ufuatiliaji wa mifumo ya e-project management, e-library, e-wakili, e-courtbroker na process server na Judicial portial na ujenzi wa kituo cha kusimamia na kuratibu mwenendo wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA (Judiciary Virtual Situation Room-VSR).

 

Kikao cha Tume kilihudhuriwa na Makamishna watano wa Tume ambao ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.Mustapher Siyani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ,Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi. Wengine ni Bw. Bahame Tom Nyanduga (Wakili wa kujitegemea) na Bi.Dosca  Mutabuzi (Wakili wa kujitegemea).


 Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Prof. Elisante Ole Gabriel (Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Katibu waTume), Bi. Eziel Mtei (Naibu Katibu wa Tume – Ajira), Bi. Alesia Mbuya (Naibu Katibu wa Tume – Maadili), na Mhe. Eva Nkya (Msajili Mkuu wa Mahakama).

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongoza kikao cha kawaida cha Tume ya Utumishi wa Mahakama jana jijini Dar es salaam. 

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa Kikao cha Tume ya Utumishi wa Mahakama jana jijini Dar es salaam. 

Sehemu ya Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakiwa kwenye kikao  cha kawaida cha Tume jana jijini Dar es salaam. Kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni