Alhamisi, 1 Agosti 2024

WELEDI NYENZO MUHIMU KATIKA KAZI: JAJI NDUNGURU

Na. LUSAKO MWANG’ONDA-Mahakama, Iringa

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe Dunstan Ndunguru amewataka watumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu wakiwa katika majukumu yao ya kuwatumikia wananchi. 

Mhe. Ndunguru ametoa wito huo jana tarehe 31 Julai, 2024 alipokuwa anazungumza na wajume wa Kikao cha Menejimenti ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Iringa. 

Mhe. Ndunguru amesema kwamba siyo vyema kwa mtumishi wa Mahakama kuwa na uadilifu unaotiliwa mashaka maana hali hiyo hushusha imani ya wananchi kwa Mahakama.

Jaji Mfawidhi ambaye kikanuni ndiyo Mwenyekiti wa Kikao hicho amesema, “imani ya wananchi ni kubwa sana kwa Mahakama, hivyo uongozi hautamfumbia macho mtu yeyote ambaye kwa namna yeyote ile atataka kuitia doa imani waliyo nayo wananchi kwa muhimili huu.

Amesisitiza kuwa kufanya kazi kwa weledi katika zama hizi ni lazima kuendane na matumizi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), maana huo ndiyo mwelekeo ambao Mahakama ya Tanzania na Nchi kwa ujumla ambao wamechagua kwenda nao.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kuu ya TanzaniaKanda ya Iringa, akiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku na Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Iringa na Njombe.

Wengine ni Watendaji wa Mahakama Iringa na Njombe, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya zote zilizopo katika Mikoa ya Iringa na Njombe na Viongozi wengine wa vitengo mbalimbali.

Kikao hicho kimetoka na maazimio mbalimbali, ikiwemo matumizi ya TEHAMA kuendelea kupewa kipaumbele katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kimahakama. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru akisisitiza jambo wakati akiongea na wajumbe wa Kikao cha Menejimenti - Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku (wa kwanza kulia) akichangia jambo wakati wa kikao hicho. 

Kaimu Mtendaji wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Bi. Dorice Kisanga akiwasilisha taarifa ya utendaji kwa Mahakama za Mkoa wa Iringa.

Mtendaji wa Mahakama ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe,  Bw. Richard Mbambe akiwasilisha taarifa ya utendaji kwa Mahakama za Mkoa wa Njombe. 

Sehemu ya wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, (juu na chini) wakifuatilia mjadala wakati wa kikao hicho.

 

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni