Ijumaa, 11 Oktoba 2024

JAJI DING'OHI AWAASA WAFUNGWA KUJISOMEA KUJUA HAKI ZAO

Na RICHARD MATASHA, Mahakama-Mtwara

Kaimu jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Saidi Ding’ohi amewaasa wafungwa kutafuta taarifa na elimu sahihi kuhusiana na haki zao hasa haki ya rufaa na nyinginezo. 

Mhe. Ding’ohi aliyasema hayo hivi karibuni katika mkutano pamoja na wafungwa wa Gereza la Kiwanda cha Chumvi mkoani Mtwara alipofanya ziara ya ukaguzi katika Gereza hilo.

“Ni vyema kutumia muda wenu kujisomea kujua haki zenu pamoja na kujifunza shughuli mbalimbali ili pindi mtakapotoka gerezani mkawe raia wema na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa,” alisema Mhe.Ding’ohi.

Katika mkutano huo, Kaimu Jaji Mfawidhi huyo alipokea taarifa mbili moja kutoka kwa Mkuu wa Gereza na nyingine kutoka kwa wafungwa zikielezea hali ya magereza pamoja na changamoto zinazokabili Gereza hilo.

Katika nyakati tofauti, Mkuu wa Gereza la Kiwanda cha Chumvi, ASP. Johstone Kayungi Kabyemela pamoja na wafungwa walipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mtwara katika shughuli ya utoaji haki, pia wameshukuru kwa ziara hiyo na kuomba watembelewe mara kwa mara haswa na Mawakili ili wajifunze zaidi kuhusu sheria za nchi.

Katika ziara hiyo, timu nzima ya haki jinai ikiongozwa na Mhe Ding’ohi walipata fursa ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza chumvi kinachomilikiwa na Gereza hilo na kupata maelezo ya kina ya namna chumvi inavyochakatwa kuanzia hatua ya awali hadi kufungashwa kwa ajili ya kuuzwa.

Katika ziara yake, Mhe. Ding’ohi aliambatana na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Seraphine Nsana, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Bw. Yusuph Msawanga, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mnzava, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mtwara, Mhe. Lucas Jang’andu, Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo, Maafisa wa Mahakama pamoja na wadau wengine wa Haki Jinai wa mkoani humo.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Saidi Ding’ohi (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Gereza Kiwanda Chumvi, ASP. Johstone Kayungi Kabyemela (kulia), Naibu Msajili Mahakama Kuu kanda ya Mtwara Mhe. Seraphine Nsana (aliyesimama kulia kwa Mhe. Ding'ohi) pamoja na wadau wengine wa Haki Jinai wakiwa mbele ya jengo la Gereza hilo hivi karibuni.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Saidi Ding’ohi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Gereza Kiwanda Chumvi, ASP. Johstone Kayungi Kabyemela (kulia), Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Seraphine Nsana (aliyesimama kulia kwa Mhe. Ding'ohi) pamoja na wadau wengine wa Haki Jinai mbele ya jengo la Kiwanda cha Chumvi.

Mkuu wa gereza Kiwanda Chumvi ASP. Johstone Kayungi Kabyemela (wa kwanza kulia) akieleza jambo kwa Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Saidi Ding’ohi na wadau wengine kuhusu mitambo iliyopo ndani ya Kiwanda cha Chumvi.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni