Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha
Kiwango cha kumaliza mashauri katika Mahakama ya Rufani Tanzania kimepanda kwa asilimia 68 katika kipindi cha Januari hadi Juni 2024 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2023 ambapo kiwango cha umalizaji mashauri kilikua asilimia 43.
Akiwasilisha Taarifa ya Mashauri ya Mahakama ya Rufani kwa kipindi cha Januari-Juni, 2024 katika Mkutano wa nusu mwaka wa Mahakama hiyo leo tarehe 10 Oktoba, 2024 jijini Arusha, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert amesema kumekuwa na ozengeko la asilimia 25 kwenye umalizaji wa mashauri katika kipindi hicho.
“Kiwango cha kumaliza mashauri kwa kipindi cha mwezi Januari-Juni 2024 kilikuwa ni asilimia 68 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023 ambapo kiwango cha umalizaji mashauri kilikua asilimia 43. Kwa takwimu hiyo tunaona kiwango hicho kimepanda kwa asilimia 25,” amesema Mhe. Herbert.
Akizungumzia kuhusu uwiano wa uondoshaji wa mashauri katika vipindi vinavyofanana kwa kwa mwaka 2023 na 2024 katika kipindi cha Januari-Juni, Msajili huyo amesema katika kipindi hicho kwa mwaka 2023, mashauri yaliyopangwa yalikuwa 933, mashauri yaliyoamjuliwa yalikuwa 765 sawa na asilimia 82 na mashauri yaliyoahirishwa yalikuwa 168 sawa na asilimia 18.
Aidha, Mhe. Herbert amesema kuwa, katika kipindi hicho Mahakama ya Rufani imefanya jumla ya vikao vinne katika Kanda 16 za Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza, Iringa, Tabora, Mtwara, Dodoma, Tanga, Kigoma, Bukoba, Zanzibar, Moshi, Morogoro, Musoma na Sumbawanga.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha Januari-Juni, 2024 mashauri yaliyopangwa yalikuwa 1,072, yaliyoamuliwa yalikuwa 941 sawa na asilimia 88 na mashauri yaliyoahirishwa yalikuwa 131 asilimia 12.
Ametaja idadi ya mashauri kwa kila jopo moja lenye Majaji watatu, kwamba lina uwezo wa kusikiliza wastani wa mashauri kati ya 26 na 33 kwa kikao kimoja.
“Hadi kufikia Juni, 2024 Mahakama ilikuwa ina jumla ya majopo 11. Iwapo majopo hayo yangeketi kwa ukamilifu wake, yalikuwa na uwezo wa kuondosha wastani wa mashauri 363 kwa kikao kimoja kwa kiwango cha juu cha mashauri 33 kwa kila jopo ambayo ni sawa na mashauri 1,452 kwa vikao vinne,” ameeleza Mhe. Herbert.
Msajili huyo amesema kuwa, hadi kufikia Juni 2024, kila jopo lilikuwa na mzigo wa mashauri 536. Idadi hiyo ikigawanywa kwa mashauri 33 yanayopangwa kwa kikao kimoja, kila jopo litahitaji vikao 16 kumaliza mashauri yote 536.
Aidha, mzigo wa mashauri kwa jopo umeendelea kupungua kutokana na kuongezeka kwa Majaji wa Rufani kutoka mashauri 722 Juni 2023 mpaka 536 kufikia Juni 2024.
Amebainisha mafanikio ya Mahakama hiyo yaliyopatikana katika kipindi cha miezi sita (Januari-Juni, 2024) kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya kumalizika kwa mashauri (clearance rate) kutoka mashauri 765 hadi kufikia 941, kupungua kwa idadi ya mashauri ya mlundikano, kupungua kwa idadi ya mashauri yanayoahirishwa.
Mafanikio mengine ni kufanyika kwa vikao vyote vinne kwa asilimia 100 kama vilivyopangwa kwa mujibu wa kalenda ya Mahakama, kuongezeka kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) usikilizaji wa mashauri, Maamuzi yote kupandishwa kwenye TanzLII.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kiutawala na kiutumishi katika Mkutano huo, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bw. Victor Kategere amesema, ili kuendana na kasi ya matumizi ya TEHAMA, Mahakama ya Rufani kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka imeanza zoezi la kudijiti majalada katika masjala zake zote lengo likiwa ni kuifikia Februari, 2025 kuwe nakala laini za majalada yote katika Vikao vya Mahakama.
Aidha, akizungumzia kuhusu mipango kadhaa ya Mahakama hiyo, Bw. Kategere amesema, wamepanga kuongeza idadi ya vikao kwa Kanda zenye mashauri mengi ya mlundikano, mfano Dar es Salaam, Mwanza, Moshi, Arusha, Musoma na Mbeya.
“Mipango mingine ni kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa Masjala Kuu pamoja na masjala ndogo zote za Mahakama ya Rufani. Katika kufanikisha hili kila Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani wamepangiwa masjala za kusimamia na kukagua,” amesema Bw. Kategere.
Mkutano huo wa siku mbili wa Mahakama wa Rufani umefunguliwa leo na Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambao pamoja na mambo mengine unalenga kujadili utendaji kazi wa shughuli za Mahakama hiyo na kuweka mikakati na maazimio ya kuboresha zaidi utendaji kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni