- Asema kazi kubwa wanayofanya inathaminiwa
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 10 Oktoba, 2024 amefungua Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani Tanzania na kuwapongeza Majaji na watumishi kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayofanya kwenye jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Prof. Juma ametoa pongezi hizo Vioingozi hao wa Mahakama kwa kuendelea na jitihada za kuendesha mashauri kwa mafanikio makubwa, licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wanapotekeleza majukumu yao kila siku.
Amesema wakati anamwapisha Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Nenelwa Mwihambi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya, hasa usikilizaji wa mashauri kwa wakati.
“Mheshimiwa Rais anasema kwamba katika safari zake za nje, alikutana na wafanya biashara na wawekezaji, wakamsifu kwa maboresho ya miundombinu…
“Alisema Mahakama imerekebishika sana na siku hizi kesi hazichukui muda mrefu, zamani watu walikuwa wanategesha mashauri katika Mahakama ya Rufani wakijua kwamba zitachukua muda mrefu, lakini sasa hivi tumeweza kufanya kazi kubwa,” amesema.
Jaji Mkuu amewaambia Majaji hao kuwa kazi kubwa wanayofanya wakati wa utekelezaji wa majukumu yao inathaminiwa na siyo mara nyingi kupata pongezi kama hizo ukilinganisha na kile kinachoandikwa kwenye mitandao ya kijamii.
Mhe. Prof. Juma ametaja moja ya changamoto mojawapo wanayokabiliana nayo ni ongezeko la mashauri ya rufani katika Mahakama ya Rufani ukilinganisha na idadi ya Majaji wanaohudumu katika ngazi hiyo.
Hivyo, amewaomba Majaji kujadili kwa pamoja kubaini mbinu bora zaidi za kushughulikia na kutatua changamoto zilizopo ili kutekeleza kwa ufanisi jukumu kubwa na muhimu la utoaji haki katika Mahakama ya Rufani ambayo ndiyo yenye jukumu la mwisho katika utoaji haki hapa nchini.
Mkutano huo unafanyika kwa ajili ya kufanya tathmini na mapitio ya shughuli za Mahakama ya Rufani kwa lengo la kuangalia walipotoka, walipo na wanakoelekea katika kutekeleza malengo ya mwaka ya Mahakama ya Rufani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni