Alhamisi, 10 Oktoba 2024

MWISHO MATUMIZI YA KARATASI MAHAKAMANI WAKARIBIA

  • Wimbi la teknolojia lasambaa kila kona
  • Mahakama Kuu Geita mfano wa kuigwa

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza Majaji wa Mahakama ya Rufani kujiandaa kuachana na matumizi ya karatasi katika shughuli za kimahakama, ikiwemo usikilizaji wa mashauri.

Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 10 Octoba, 2024 alipokuwa anafungua Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani Tanzania 2024 unaofanyika katika Hoteli ya Mount Meru jijini hapa.

Jaji Mkuu ameeleza kuwa Mahakama ya Rufani haijachukua nafasi yake ya uongozi kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ukilinganisha na Mahakama za chini, hususan Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, ambayo haitumii kabisa karatansi. 

“Tahadhali ambayo inajitokeza ni kwamba yale mashauri ambayo yamesajiliwa katika mfumo mpya yanakaribia kufika Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu Kanda ya Geita hawatumii kabisa karatasi. Lakini sisi Mahakama ya Rufani tumebaki nyuma, hatuna utayari na uwekezaji mkubwa umefanywa kwenye mifumo ya TEHAMa,” amesema.

Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa anafahamu Msajili wa Mahakama ya Rufani yupo katika hatua ya kupitia kanuni za Mahakama ya Rufani ili kuona kama zinaendana na ili kusiwe na changamoto za kikanuni katika kushughulikia mashauri ya rufaa zinazotoka katika Mahakama za chini ambazo zilisikilizwa kwa njia ya Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri wa Ki-elektroniki (e-CMS).

Jaji Mkuu amebainisha kuwa Mahakama Kanda ya Geita imekuwa mfano mzuri katika matumizi ya teknolojia kwa kuacha kutumia karatasi kuanzia tarehe 22 Novemba, 2023 ilipoanzishwa, huku sunami la matumizi ya teknolojia likisambaa kwenye Mahakama mbalimbali nchini.

“Ukienda Geita hakuna karatasi na wananchi wameshaelewa na ndiyo maana nilimwomba Msajili wa Mahakama ya Rufani awapeleke Maafisa Kumbukumbu wetu wakatembelee Geita, waone wanavyofanya kazi, ni kwa namna gani wamehama kabisa katika mfumo wa kutegemea makaratasi na wapo katika mfumo wa kidijitali kwa asilimia 100,” amesema.

Mhe. Prof. Juma amewakumbusha kuwa Mahakama ya Tanzania haitarudi nyuma katika matumizi ya teknolojia katika shughuli zote za kimahakama, hivyo kila mmoja anapaswa kujiandaa kutumia uwekezaji mkubwa huo ambao umefanyika kupitia mradi wa Benki ya Dunia. 

“Kwa bahati nzuri tumeshapitia mafunzo mengi ya e-CMS tumetoa mchango wetu, tumechangia katika kuufundisha mfumo huu, tujitayarishe sasa ili tuwe tayari kupokea mashauri ambayo yanatoka Mahakama za chini ambazo zimekubali maboresho,” amesema.

Jaji Mkuu ameeleza pia kuwa katika nafasi zao za kiuongozi, Majaji wa Mahakama ya Rufani ni muhimu kufuatilia kwa ukaribu ni kwa kiasi gani Akili Bandia (Artificial Intelligence) inavyobadili Dunia, itaboresha au kubadili kazi za utoaji haki Tanzania. 

Amefafanua kuwa tayari Mahakama ya Tanzania inatumia Artificial Intelligence katika mifumo mbalimblai, ikiwemo e-CMS, Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS), Primary Courts App, Mahakama Mtandao (Video Conferencing), e-Learning Platform, TANZLII na kadhalika. 

Mahakama ya Tanzania ianaendelea na jitihada za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika mfumo wa utoaji haki, huku ngazi za chini za kimahakama zikipiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA hususan e-CMS.

Mkutano huo unafanyika kwa lengo la kukutana kwa ajili ya kufanya tathmini na mapitio ya shughuli za Mahakama ya Rufani na kuangalia walipotoka, walipo na wanakoelekea katika kutekeleza malengo ya mwaka ya Mahakama ya Rufani Tanzania.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anafungua  Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani Tanzania 2024 leo tarehe 10 Octoba, 2024 jijini Arusha.


Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya  Rufani Tanzania (juu na chini) ikimsikiliza Jaji Mkuu katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.



Sehemu nyingine ya Majaji wa Mahakama ya  Rufani Tanzania (juu na chini) ikimsikiliza Jaji Mkuu katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.


Sehemu nyingine ya tatu ya Majaji wa Mahakama ya  Rufani Tanzania (juu na picha mbili chini) ikimsikiliza Jaji Mkuu katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.




Sehemu ya  Makatibu wa Majaji wa Mahakama ya  Rufani Tanzania, Viongozi wa Mahakama na watumishi wengine (juu na picha mbili chini) ikimsikiliza Jaji Mkuu katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.



Washiriki wa Mkutano wakifuatilia kwa makini.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni