Jumatano, 9 Oktoba 2024

MAHAKAMA IRINGA YAAZIMIA KUVUKA MWAKA BILA MASHAURI YA MLUNDIKANO

Na LUSAKO MWANG’ONDA, Mahakama - Iringa

Menejimenti ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa imeazimia kuumaliza mwaka 2024 bila kuwa na mashauri ya mlundikano (backlog). 

Akizungumza na wajumbe wa Kikao cha Menejimenti ya Kanda hiyo katika ukumbi wa Mahakama hiyo leo tarehe 09 Oktoba, 2024, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru amesema kila Jaji na Hakimu katika Kanda hiyo ahakikishe hawi na mashauri ya mlundikano ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

“Naomba kuwasisitiza Waheshimiwa wote kuwa kila mtu ahakikishe ndani ya kipindi hiki kilichobaki kuukamilisha mwaka huu, kila mmoja wetu ahakikishe anamaliza mashauri yote ya muda mrefu ili ifikapo Desemba wote kwa pamoja tuvuke pasipo kuwa na mlundikano wa mashauri. Nataka Kanda yetu ya Iringa mwaka huu tuumalize pasipo kuwa na viporo vilivyochacha,” amesema Mhe.Ndunguru.

Jaji Ndunguru ambaye kikanuni ndio Mwenyekiti wa Kikao hicho ameongeza kwa kusema kuwa, “Mahakama Iringa ni lazima tuuishi kwa vitendo ule msemo wetu wa ‘Justice delayed is justice Denied’ yaani Haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa.”

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwasisitiza wajumbe wa kikao hicho kuhusu uhuishaji wa mashauri kwa wakati katika Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS). Amesema hatamani kuona Kanda yake kuwa moja ya Kanda ambazo mashauri hayahuishwi kwenye Mfumo kwa wakati na hivyo amewataka kila mmoja awajibike kwa kadri impasavyo kuwajibika.

Kadhalika, Mhe. Ndunguru amesisitiza pia kufanya kazi kwa weledi katika zama hizi na kwamba ni lazima kuendana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), maana huo ndiyo mwelekeo ambao Mahakama ya Tanzania na nchi yetu kwa ujumla tuliochagua kwenda nao.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa akiwemo Naibu Msajili, Mhe. Bernazitha Maziku, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Iringa na Njombe, Watendaji wa Mahakama Iringa na Njombe, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya zote zilizopo Mikoa ya Iringa na Njombe na viongozi wengine wa Vitengo mbalimbali.

 Maazimio ya kikao hicho ni pamoja na kuendelea kuweka kipaumbele katika matumizi ya (TEHAMA) katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kimahakama. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (kushoto) akisisitiza jambo wakati akiongoza Kikao cha Menejimenti ya Mahakama hiyo kilichofanyika leo tarehe 09 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Mahakama hiyo. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku (wa kwanza kushoto) akichangia jambo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Mahakama hiyo. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa.


Afisa Utawala wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bw. Noel Shao akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama za Mkoa wa Iringa kwa niaba ya Mtendaji wa Kanda hiyo, Bi. Melea Mkongwa.  

Sehemu ya wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa wakifuatilia kinachojiri katika kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni