Jumanne, 29 Oktoba 2024

JAJI KIONGOZI AFANIKIWA KUTETEA TASNIFU YAKE YA UZAMIVU CHUO KIKUU CHA DODOMA

  ARAPHA RUSHEKE na JEREMIA LUBANGO, Mahakama - Dodoma.

 

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani ambaye ni Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Kitivo cha Sheria, jana tarehe 28 Oktoba, 2024 ameandika historia ya mafanikio katika safari ya kitaaluma baada ya kutetea kwa ufanisi tasnifu yake ya Shahada ya Uzamivu (PhD).

 

Tasnifu iliyowasilishwa na Jaji Kiongozi ilihusu “Uchunguzi wa Changamoto za Kisheria na Utekelezaji zinazo athiri Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri katika Utoaji Haki kwa wakati kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania.

 

Utetezi huo uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma na kudumu kwa takribani saa tatu, ulishuhudiwa na watazamaji wengi waliokuwepo ukumbini na wale waliofuatilia kupitia mtandao, ambapo Mhe. Siyani aliwasilisha kwa umahiri mkubwa matokeo ya utafiti wake na kutoa majibu ya kina kwa maswali yote kutoka kwa jopo la Wahadhiri lililongozwa na Prof. Adam B. S Mwakalobo.

 

Utafiti wa Mhe. Siyani ulilenga kuchunguza Changamoto za Kisheria na Utekelezaji zinazoathiri Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri katika Utoaji Haki kwa wakati kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania na uliwavutia wahudhuriaji wengi kwa sababu ya umuhimu wake katika kuboresha eneo muhimu la upatikanaji wa haki kwa wakati.

 

Baada ya majadiliano ya kina Mwenyekiti wa jopo hilo, Prof. Mwakalobo, alitangaza kuwa Mhe. Siyani amefanikiwa kwa kiwango cha juu kutetea tasnifu yake, huu ni ushindi mkubwa kwa Mhe. Siyani na hatua muhimu kuelekea kukamilisha safari yake ya Shahada ya Uzamivu (PhD).

 

Kwa upande wake Mhe. Siyani ameelezea jinsi safari yake ya masomo iliyochukua takribani miaka mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi kufikia tamati hiyo. “Utafiti wangu ulilenga kuondoa changamoto ya msongamano wa mashauri yaliyoko Mahakama Kuu kwa maana ya kuona namna ambavyo Sheria zilizopo Mahakama Kuu zina mapungufu na jinsi gani zinaweza kuboreshwa ili kuharakisha mchakato wa utoaji haki kwa wale wanaokuja mahakamani kwa ajili ya kupata haki” amesema Jaji Kiongozi Mhe. Siyani.

 

Kadhalika, Mhe. Siyani amekipongeza Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa kwa wanafunzi wakati wote wa masomo yao, kitu kilichohakikisha safari yake inatamatika ndani ya muda mfupi wa miaka mitatu.

 

Pamoja na Prof. Mwakalobo, wahadhiri wengine waliounda jopo la watahini katika utetezi huo, ni Dkt. Daudi Francis Momburi, Dkt. Elia Mwanga, Dkt. Peter Shughuru, Dkt. Baraka Mkami, na Dkt. Ryoba Marwa. Miongoni wa waliohudhuria utetezi huo ni Dkt. Kulwa Gamba ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa Mhe. Siyani, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Dkt. Juliana Masabo, Amidi wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma,Dkt. Ines Kajiru, wanafunzi wa sheri wa chuo kikuu hicho  na Watumishi mbalimbali wa Mahakama.


Picha ya juu na chini Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Mustapher  Mohamed Siyani akiwasilisha utetezi wake jana tarehe 28     Oktoba, 2024 katika jopo uliiofanyika katika ukumbi wa CIVE uliopo Chuo Kikuu cha  Dodoma (UDOM).




Mwenyekiti wa Jopo hilo Prof.Adam B.S Mwakalobo akimuuliza swali Mhe.Siyani wakati wa kutetea tasnifu ya Uzamivu wake.



Jopo pamoja na wafuatiliaji waliohudhuria wakati  Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Mustapher  Mohamed Siyani   Mhe.Siyani akitetea Shahada yake ya Uzamivu iliyofanyika katika ukumbi wa CIVE uliopo katika chuo cha UDOM.


Jopo pamoja na wafuatiliaji waliohudhuria wakati  Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Mustapher  Mohamed Siyani   Mhe.Siyani akitetea Shahada yake ya Uzamivu iliyofanyika katika ukumbi wa CIVE uliopo katika chuo cha UDOM.




Jaji Kiongozi Mahakama ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (aliyevaa miwani) akipeana mikono na mmoja wa “supervisor” wake Dkt.Kulwa Gamba.

 


Jaji Kiongozi Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa     sita kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja jopo na wajumbe waliohudhuria kwenye utetezi wa Shahada ya Uzamivu (PHD). kutoka kushoto ni Dkt. Daudi Francis, Dkt. Elia Mwanga, Dkt. Peter Shughuru, Dkt. Juliana Masabo, Prof. Adam Mwakalobo, Dkt. Ines Kajiru,Dkt.Baraka Mkami, Dkt. Ryoba Marwa na Dkt. Kulwa Gamba.

    (Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni