Jumanne, 29 Oktoba 2024

MAHAKAMA KANDA YA MOROGORO YAZINDUA WIKI YA UTUNZAJI WA MAZINGIRA

Na EVELINA ODEMBA – Mahakama Ulanga, Morogoro

 

Mahakama ya Tanzania Kanda ya Morogoro hivi karibuni ilizindua Wiki ya Utunzaji wa Mazingira kwa Mahakama zote zilizopo katika Kanda hiyo.

 

Uzinduzi huo ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala katika hafla fupi kwenye viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.

 

Mhe. Kilakala alitoa pongezi kwa Viongozi na watumishi wa Mahakama kwa kuibeba ajenda ya mazingira kwa kupanda miti ambayo ni kiini cha uhai.

 

 Aliendelea kueleza kuwa jitihada hizo zisiishie katika mazingira ya Mahakama pekee bali zisambae pia katika mazingira ya nyumbani ili kuweka uwiano sawa wa mazingira mahali pa kazi na mahala pa makazi.

 

“Nawapongeza sana kwa kupendezesha Mahakama zetu, eneo hili linapendeza, linavutia na kijani kinaonekana. Tunatamani kuona hali hii inafanana na mazingira mahala tunapoishi,” alisisitiza Mhe. Kilakala na kuongeza kuwa ni vyema kila mmoja akawa Balozi wa kutoa elimu ya mazingira kwa kuwa eneo hilo ni changamoto kwa Mkoa wa Morogoro.

 

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor alisema kuwa licha ya kuwa kazi ya utunzaji wa mazingira sio rahisi, Mahakama Kanda ya Morogoro imejitahidi kuendelea kuyalinda na kuyaboresha bila kuathiri jukumu lake la msingi la kutoa haki sawa na kwa wakati.

 

“Mbali na maadhimisho ya pamoja ya Siku ya Mazingira Kitaifa, sisi Kanda ya Morogoro tumetenga siku yetu maalumu ili kuendelea kudumisha utunzaji wa mazingira. Kama inavyoonekana hapa katika jengo letu, tuna bustani nzuri ya maua na miti, hii ni juhudi maalumu ya kuhakikisha mazingira ya Mahakama zetu zote yanakuwa na muonekanao wa kuvutia,” alisema. 

 

Uzinduzi wa Wiki ya Mazingira ulihudhuliwa na Viongozi mbalimbali, wakiwemo Majiji wa Mahakama Kuu, Mhe. Amir Mruma na Mhe. Stephen Magoiga, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni, Naibu Wasajili, Mhe. Fadhili Mbelwa na Mhe. Susan Kihawa.

 

Alikuwepo pia Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Asha Waziri, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya pamoja na watumishi wa Mahakama.

 

Katika uzinduzi huo jumla ya miti 60 ilipandwa na zoezi hilo litaendelea kwa kukamilisha kupanda miti isiyopungua 200 kabla ya kumalizika kwa mwezi Desemba 2024.



Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala akipanda miti kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Mazingira kwa Mahakama Kanda ya Morogoro. 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akipanda mti wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Mazingira kwa Mahakama Kanda ya Morogoro.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma akishiriki zoezi la kupanda miti.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Stephen Magoiga akishiriki zoezi la utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti.



Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni akishiriki zoezi la kupanda miti.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Susan Kihawa akishiriki kupanda miti.


Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Nunge wakishiriki kupanda miti.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akikabidhi cheti cha kuuthamini mchango wa utunzaji wa mazingira kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kilosa, Mhe. Agnes Ringo.



Matukio katika picha wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Mazingira kwa Mahakama Kanda ya Morogoro (picha juu na mbili chini).


  

 

 Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni