Mashauri 11 yasikilizwa na kuamuliwa ndani ya siku sita
Na KANDANA LUCAS-Mahakama Kuu Musoma
Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania laendelea kuendesha kikao (session) katika Masjala ndogo ya Mahakama hiyo iliyopo Mahakama Kuu Musoma.
Akizungumza na wadau mbalimbali wakati wa kikao cha ufunguzi (pre-session meeting) tarehe 28 Oktoba,2024 Mwenyekiti wa jopo hilo, Mhe. Stella Mugasha, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama hiyo, ametoa rai kwa wadau wote wanaohusika na mashauri yaliyopangwa Kenosha ushirikiano ili kuhakikisha mashauri yote yaliyopangwa yanasikilizwa na kuamuliwa kwa wakati.
“Nawashuruku wadau wote waliohudhuria kwenye kikao hiki muhimu cha kufungua rasmi kikao cha Mahakama ya Rufani hapa Musoma, aidha niwaombe wote wanaohusika na mashauri yaliopangwa kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha wakati wa kikao hicho ili kutimiza lengo kwa ufanisi,” Mhe Jaji Mugasha amesema.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Joseph Fovo wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya kikao hicho, amesema kwamba hadi kufikia tarehe jana jumla ya mashauri kumi na moja (11) yamesikilizwa na kuamuliwa kati ya mashauri 26 yaliyopangwa kusikilizwa.
“Kasi ya usikilizwaji wa mashauri ni nzuri kwani kwa muda wa siku sita za kwanza, Wahe. majaji wamefanikiwa kumaliza mashauri kumi na moja kati ya 26, hivyo ni matarajio yetu kuwa mashauri yote yaliyopangwa yataisha ndani ya muda uliowekwa”Mhe.Fovo,” amesema.
Kikao hicho kilianza rasmi tarehe 21 Oktoba, 2024 huku kikitarajiwa kuhitimishwa tarehe 8 Novemba, 2024 na kinaendeshwa na jopo la majaji wanne, ambao ni Mhe.Stella E.Augustine Mugasha (Mwenyekiti), Mhe Ignas Paul. Kitusi, Mhe.Dkt. Lilian Leonard Mashaka, na Mhe. Abdul-Hakim Ameir Issa.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya aliwakaribisha majaji hao na kuwaahidi ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watumishi wa Mahakama hiyo katika kipindi chote cha kikao hicho.
“Sisi viongozi na watumishi wa Kanda ya Musoma, tunawakaribisha sana majaji wa Mahakama ya Rufani na watumishi wengine waliombatana nao na tunaahidi ushirikiano wa kutosha kadri itakavyohitajika wakati wote wa kikao ili kuwezesha usikilizwaji wa mashauri kufanyika katika mazingira rafiki na tulivu,” amesema Mhe. Mtulya.
Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, wakiongozwa na Mhe. Jaji Stella Augustine Mugasha (aliyetangulia) wakisalimiana na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma baada ya kuwasili katika viwanja vya Mahakama Kuu Musoma kuanza rasmi kikao cha Mahakama ya Rufani.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Joseph Fovo (aliyesimama), akiwasilisha taarifa kwa majaji na wadau (hawapo pichani) kuhusu kikao cha Mahakama ya Rufani wakati wa kikao cha ufunguzi (Pre-session meeting).
Mwenyekiti wa jopo Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Stella Augustine. Mugasha (katikati) akizungumza na wadau mbalimbali (hawapo pichani) wakati wa kikao cha ufunguzi (pre-session meeting).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya (aliyenyoosha mkono) akiwatambulisha watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma (hawapo pichani) baada ya kuwapokea majaji wa Mahakama ya Rufani katika viwanja vya Mahakama Kuu Musoma.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni