Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amefika msibani kumpa pole Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel nyumbani kwao Suye Oloirien Mkoani Arusha kufuatia kifo cha Mama mzazi wa Prof. Ole Gabriel kilichotokea tarehe 29 Septemba, 2024.
Jaji Kiongozi aliambatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Claud Mugeta tarehe 01 Oktoba, 2024 ambapo walipata fursa ya kusaini kitabu cha maombolezo ya marehemu Naitovuaki Mosses Lengutai na kujumuika na waombolezaji wengine waliofika msibani pale kwa lengo la kuwafariji wafiwa.
Mhe. Siyani pamoja na Mhe. Mugeta walilakiwa na Prof. Ole Gabriel na kupata muda wa kuwasalimia na kuwafariji wafiwa na waombolezaji wengine waliokuwepo msibani hapo.
Maandalizi ya mazishi yanaendelea kufanyika nyumbani kwa Marehemu na mazishi yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi tarehe 05 Oktoba, 2024.
Kwa mujibu wa ratiba, safari ya kuelekea katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Moshono itaanza saa 3:30 asubuhi kwa ajili ya ibada na waombolezaji wataanza kuaga mwili wa marehemu na kutoa salamu zao za mwisho kuanzia saa 3:45 asubuhi hadi saa 7:00 mchana.
Baada ya Ibada, salamu za rambirambi zitatolewa kutoka kwa watu, vikundi na Taasisi mbalimbali kwa watakaohudhuria kanisani na baadae kuelekea nyumbani tayari kwa mazishi. Salamu za rambirambi zitatolewa pia baada ya mazishi nyumbani kwa marehemu.
Mahakama ya Tanzania inaungana na ndugu, jamaa na marafiki kuomboleza msiba huu, Bwana alitoa na Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni