Alhamisi, 3 Oktoba 2024

WATUMISHI WA MAHAKAMA KUU KANDA YA GEITA WAPATA MAFUNZO YA KUWAONGEZEA UJUZI


    Na CHARLESI NGUSA- Mahakama, Geita.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina  amesema Kanda hiyo imeandaa mafunzo ya afya ya akili na udhibiti wa masongo wa mawazo, ikiwa lengo la Mahakama la kuhakikisha watumishi na wadau wanapata mafunzo mbalimbali ili kuendana na ukuaji wa teknolojia na mabadiliko ya sheria.

 

Mhe. Jaji Mhina alisema hayo hivi karibuni wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika ukumbi wa Mahakama Kuu  Kanda ya Geita.

 

 “Tunapoendelea na shughuli zetu za usikilizaji wa mashauri, ni muhimu kuhakikisha kuwa tunao uelewa mkubwa  wa sheria na matumizi ya mifumo yetu ya uendeshaji ili tuweze kuwahudumia wateja wetu kwa ubora; na ndiyo maana ni muhimu kuendelea kupata mafunzo haya ili tuweze kubadilishana uzoefu kutoka katika maeneo yetu ya kazi tukishirikiana na wawezeshaji wetu hawa. Hivyo, nawakaribisheni  katika mafunzo haya ili kuweza kujiongezea ujuzi katika utendaji wetu wa kila siku,” alisema  Jaji Mhina.

 

 Mafunzo hayo yalihudhuriwa na watumishi wa Mahakama, wadau mbalimbali  wakiwemo Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Madalali wa Mahakama na Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Mkoa wa Geita. 

 

Katika mafunzo hayo, wawezeshaji mbalimbali walialikwa kwa ajili ya kuwasilisha mada   za   kuwaongezea ujuzi watumishi hao. Walioalikwa kutoa mada katika mafunzo hayo ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Jaji Cyprian Phocus Mkeha aliyewasilisha mada kuhusu Mashauri ya Utekelezaji (Execution), alisema kuwa mashauri hayo yanapaswa kuendeshwa kwa makini  ili kuepuka kuumiza upande wowote na hasa uzingatiaji wa sheria. Kwa namna nyingine lazima pia kutumia busara katika kupima kwani sheria pekee haiwezi kuamua mambo yote. 

 

“Ni muhimu kuwa na ufahamu wa sheria unazozitumia katika mashauri ya utekelezaji kwani ndiyo zana yako ya kazi muda wote na kwamba sheria unayoitumia isikinzane na sheria mama na ni vyema kujiridhisha kuwa maombi yaliyowasilishwa yanatekelezeka”, alisema Mhe. Jaji Mkeha.

 

 Daktari Bingwa wa Magojwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Garvin Nathaniel Kweka aliyewasilisha mada ya afya ya akili na namna ya kudhibiti msongo wa mawazo, ambapo. Kweka, aliwaambia watumishi hao kuwa tafiti za hivi karibuni zinaonesha kuwa Mkoa wa Geita una changamoto kubwa  ya wagonjwa wa afya ya akili. 

 

“Hii ina kutokana na matukio makubwa ya ukatili kama mauaji na kujeruhi yanayoendelea kujitokeza kila siku.Afya ya Akili inachangiwa  na mambo mbalimbali ikiwemo suala la malezi na makuzi ya mtu, hali ya mtu mwenyewe (Mood), Sonona na ulevi. Kwa ufupi: Afya ya akili inachagiwa na mzunguko wa maisha ya jamii yote,” alisema Dkt. Kweka.”

 

Aidha Dkt. Kweka alisisitiza kuwa ili mwanadamu akamilike  anahitaji mambo  makuu matano ambayo ni Afya ya mwili, mahusiano, hisia (mood), dini na afya ya akili. Kwa mantiki hiyo, ni vizuri kila mmoja kuhakikisha anajiepusha na vihatarishi vya afya ya akili kama vile ulevi uliopitiliza na sonona.

.

Muwezeshaji mwingine ni  Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Mahakama ya Wilaya Temeke Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Mhe. Sifa Jacob Kabisa aliwasilisha mada kuhusu mashauri ya mirathi na ndoa,alisema kuwa ni muhimu  katika uendeshaji wa mashauri hayo kusikiliza kwa makini na uzingatiaji wa sheria kwani tusipofanya hivyo tunaweza kusababisha wanufaika wa mirathi kupoteza haki zao na hasa watoto ambao ndiyo wategemezi wakubwa katika mashauri hayo.

 

Watoa mada wengine ni  Kaimu Meneja wa Kanda kutoka Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),Ofisi ya Geita Bw.Thomas Abdalllah Labi,ambaye alisema huduma zitolewazo na mfuko huo ikiwa ni pamoja na mapinduzi makubwa yaliyofanywa na mfuko ya matumizi ya mifumo katika kutoa huduma. Mfano kuomba madai ya mafao kwa watumishi ambayo kwa sasa haimlazimu Mtumishi kufika tawini kuwasilisha nyaraka zake bali kwa sasa mtumishi mwenyewe anaweza kujihudumia kwa kutumia mfumo wa “PSSSF Member Portal” na huduma ikakamilika. 

 

Alizitaja huduma zingine ni  kuanzishwa kwa “PSSSF Kiganjani” huduma inamwezesha mtumishi kuangalia taarifa zake kwa kutumia simu yake ya mkononi na “PSSSF Member Portal” inayomwezesha mtumishi kujisajili na kuomba mafao yake mbalimbali.

Naibu Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa  Geita, Bw. Azza Elinisamehe Mtaita aliwasilisha mada katika mafunzo hayo na Afisa Mahusiano kutoka benki ya NMB Tawi la Geita,  Bi. Suzan Wildard Mfinanga,

aliwasilisha mada kwa watumishi ya huduma zitolewazo na benki hiyo.

 

Huduma hizo ni pamoja na mikopo kwa watumishi wa umma yenye riba nafuu na kwa muda mrefu wa hadi miaka kumi, mikopo ya nyumba, mikopo ya biashara, mikopo ya elimu, mikopo ya dharula na huduma za uwakala wa benki ya NMB ambayo ni fursa kwa watumishi wa Umma katika kujiongezea kipato. 

 

Aidha, alisisitiza kuwa kwa sasa mtumishi wa Umma hana ulazima wa mshahara wake kupitia benki ya NMB ndipo apatiwe mkopo kama ilivyokuwa hapo awali, hivyo kitu cha muhimu ni kuwa na akaunti ya NMB tu ambayo ataweza kukuwekea fedha  zake alizozikopa.

 

Baadhi ya Watumishi walioshiriki mafunzo hayo walimshukuru Mwajiri kwa kuandaa mafunzo hayo na waiomba mafunzo ya namna hiyo yawe yanatolewa mara kwa mara kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuimarisha utendaji wao wa kazi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe.Kevin David Mhina akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya  Biashara, Mhe. Cyprian Phocus Mkeha akiwasilisha mada yake kwa watumishi na wadau mbalimbali waliohudhuria mafunzo hayo.


Daktari Bingwa wa Magojwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Garvin Nathaniel Kweka akiwasilisha mada yake.


Watumishi na wadau mbalimbali wakiendelea kufuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa .

 

(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo-Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni