* Wahe. Majaji na viongozi wengine wa Kanda waongoza watumishi kwenda Ngorongoro.
Na KANDANA LUCAS –Mahakama, Musoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya, amewaongoza watumishi wa Mahakama wa Kanda hiyo, kufanya ziara ya utalii iliyofanyika hivi karibuni katika Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (Ngorongroro Crator) mkoani wa Arusha.
Akizungumza na watumishi kwa nyakati tofauti wakati wa maandalizi na hitimisho la ziara hiyo, Mhe. Mtulya alieleleza lengo la ziara hiyo ni kutambua maeneo mapya ambayo watumishi wengi hawajawahi kuyafikia, kupata furaha na kuimarisha afya ya akili.
“Wafanyakazi wengi hukabiliwa na matatizo au magonjwa ya afya ya akili wakati wakiwa kazini au punde tu wanapostaafu kutokana na aina ya majukumu wanayotekeleza na muda mwingine ni kutokana na matarajio makubwa waliyonayo pale wanapoajiriwa na yasipotimizwa, wengi huambulia maradhi ya afya ya akili…
“Ili kubiliana na uwezekano wa kutokea matatizo hayo, watumishi hawana budi kufanya mazoezi ya mwili pamoja na kuwa na furaha ambapo utalii ni sehemu ya kuipata furaha hiyo,” Mhe.Jaji n Mtulya alisema.
Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Marlin Komba aliwapongeza watumishi wote waliofanikiwa kushiriki ziara hiyo na kuwashauri watumishi ambao hawakushiriki, wawe mstari wa mbele pale itakapotokea safari ya namna hiyo.
“Nawapongeza watumishi wote (Watalii wenzangu) waliofanikiwa kusafiri kwa ajili ya utalii na nawashauri wengine ambao hawakushiriki wajitahidi wakati mwingine itakapotekea ziara ya namna hii waweze kushiriki,”Mhe. Jaji Komba alisema.
Vilevile Mwenyekiti wa kamati ya safari hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Donaldo Sondo kwa upande wake aliwashukuru watumishi kwa ushirikiano wao, viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa kutoa kibali cha kusafiri nje ya Kanda.,
Naye mwakilishi wa watumishi hao, alimshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. John Rugalema Kahyoza na viongozi wengine wa Kanda hiyo, wakiwemo watumishi wote wa Mahakama ya Wilaya Karatu kwa ushirikiano waliuonesha wakati wa maandalizi ya ziara hiyo na kipindi cha utalii.
Safari hiyo ilihusisha jumla ya watumishi 46 wa kada tofauti tofauti kutoka Mahakama za ngazi mbalimbali wakiwemo Naibu Wasajili, ambao ni Mhe. Salome Mshasha, Mhe. Monica Ndyekobora na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Bw.Leonard Maufi.
Aidha ziara hiyo ya utalii ni mwendelezo wa mkakati wa Kanda wa kutembelea vivutio vya utalii nchini angalau mara moja kwa mwaka ambapo mwaka 2023, baadhi ya watumishi walitembelea mbuga ya Wanyama Serengeti.
Muonekeno wa wanyama katika Bonde la Ngorongoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya (mwenye kofia aliyesimama katikati) akifurahia jambo na watumishi wakati wa kuanza safari ya utalii iliyoanzia katika viwanja vya Mahakama Kuu Musoma.
Baadhi ya watumishi wakiwa tayari kuanza safari ya utalii.
Viongozi na Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma wakiwa kwenye picha ya pamoja pembeni mwa ziwa lilipo katika Bonde la Ngorongoro
Picha ya watumishi wakiwa kwenye lango la kuingia kwenye eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Watumishi wakiwa kwenye picha ya pamoja na watalii wengine kutoka nje nchi.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni