Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Arusha
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewashukuru waombolezaji waliofika katika msiba wa Mama yake mzazi marehemu Naitovuaki Mosses Lengutai aliyefariki dunia tarehe 29 Septemba, 2024 jijini Arusha.
Zoezi la kuaga mwili limefanyika Moshono jijini Arusha leo tarehe 04 Oktoba, 2024 likitanguliwa na ibada iliyoongozwa na Watumishi wa Mungu na kuhudhuriwa na waombolezaji waliongozwa na Majaji, viongozi, menejimenti na watumishi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania, viongozi wa dini, Asasi za Kiserikali na za kiraia, ndugu, jamaa na marafiki.
“Kwa niaba ya wanafamilia wote ninawashukuru sana majirani, viongozi mbalimbali wa kiroho, Mahakama na watumishi wake mliofika na kujumuika nasi kutupa faraja kubwa kiasi hiki, pamoja na kushiriki shughuli zilizopo. Binafsi nimekuwa nikitoa faraja, lakini, wakati mwingine inakuwa ngumu kidogo kupokea faraja lakini mmekuwa faraja sana kwa familia yetu Mungu awabariki sana,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Akizungumza katika ibada hiyo, naye Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dkt. Owdenburg Mdegela amesifu utu, wema, upendo, malezi na mwenendo mwema wa marehemu wakati wa uhai wake huku akiwaasa wanajamii kufauata mfano mzuri aliounesha wakati wa uhai wake.
“Mama yetu alikuwa ni mlezi mwema mwenye utu wema upendo na alipenda watu na Mungu, aliishi kwa kufuata njia na matendo yanayompendeza Mungu”. amesema Dkt.Mdegela.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Arusha amesema kuwa, sifa zilizotajwa kwa Mama zinatosha kuwa kilelezo cha mpenda amani, kama ambavyo jumuiya hiyo imekuwa ikisisitiza.
“Sifa nyingi zimetajwa kumhusu Mama yetu ikiwemo kupenda amani, hiyo ndiyo kazi kubwa ya jumuiya yetu. Ninawaomba ndugu waombolezaji tuendelee kumuombea na kushikamana na familia hii kuwapa faraja” amesema Mwenyekiti huyo.
Ibada ya mazishi ya Mama mzazi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama itafanyika tarehe 05 Oktoba, 2024 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Moshono kuanzia saa 2:00 asubuhi na mazishi yatafanyika katika makaburi ya familia yaliyopo Oleireini jijini Arusha.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiaga mwili wa mama yake mzazi aliyefariki dunia tarehe 29 Septemba, 2024 jijini Arusha. Wengine ni baadhi ya waombolezaji waliofika leo tarehe 04 Oktoba, 2024 katika ibada ya kuaga mwili wa marehemu Naitovuaki Mosses Lengutai.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa ameshika kwa uchungu jeneza lenye mwili wa mama mzazi aliyefariki dunia tarehe 29 Septemba, 2024 jijini Arusha.
Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dkt. Owdenburg Mdegela akitoa sala wakati wa zoezi la kuuaga mwili wa mama mzazi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akiaga mwili wa mama mzazi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama aliyefariki dunia tarehe 29 Septemba, 2024.
Mwenza wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Bi. Marina Juma (kulia) na Mwenza wa Jaji Mkuu Mstaafu, Bi. Sada Chande (kushoto) pamoja na waombolezaji wengine wakiwa katika ibada ya kuaga mwili wa marehemu Naitovuaki leo tarehe 04 Oktoba, 2024 jijini Arusha.
(Picha na MARY GWERA, Mahakama)
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni