Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha
Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kumzika mama mzazi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, marehemu Naitovuaki Mosses Lengutai aliyepumzishwa leo tarehe 05 Oktoba, 2024 katika makaburi ya familia yaliyopo Suye Oloirien jijini Arusha.
Ibada ya mazishi hayo imefanyika katika kanisa la KKKT Moshono na kuongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Magharibi Kati Tabora, Dkt. Kisiri Laizer na kuhudhuriwa na baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Wasajili na Watendaji wa Mahakama pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali, ndugu, jamaa na marafiki.
Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Dkt. Laizer ametoa pole kwa familia ya marehemu Mwinjilisti Gabriel kwa kuondokewa na Mama ambaye alikuwa mtu muhimu katika familia na kwa wengi.
Askofu Laizer, amewasihi waombolezaji wote walioshiriki katika ibada hiyo kutokata tamaa hata kama wanapita katika mambo magumu kiasi gani.
“Neno la Mungu linasema shukuruni kwa kila jambo, hata kama tunapita katika mambo magumu lakini Yesu yupo upande wetu kutushindia,” amesema Askofu huyo.
Ameongeza kwa kuwakumbusha waumini kuwa, kifo kipo wakati wote hivyo, ni muhimu kila mmoja kuishi katika na imani na kuwa mienendo sahihi inayompendeza Mungu.
“Yapo majaribu Mungu anayaruhusu ili yatujenge kiimani, tunapokutana na magumu, Yesu anarejesha furaha yetu. Katika msiba huu tunamuhitaji Yesu pekee na si msiba huu tu bali katika maisha yetu yote,” amesisitiza.
Amewataka watoto wa marehemu kuwa na mshikamano kati yao, Kaka mkubwa aongoze vema familia
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa hisia zake kuhusu msiba wa mama yake amewasihi wenye wazazi, baba na mama kuishi nao vizuri na si tu wazazi bali watu wote wanaowazunguka kwa kuwa ni baraka kubwa.
“Kufiwa ni jambo la kawaida likiwa sio kwako ila likikufika utaelewa jinsi gani inaumiza, kwakweli niliposikia taarifa za kifo cha mama nilisikia maumivu kichwani utosini, mama ni mama tu pengo lake halizibiki kwakuwa ni mtu muhimu, hakuna mama wawili duniani,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Amewakumbusha waombolezaji mambo matano muhimu ya kuzingatia wanapopata msiba kuwa ni pamoja na kufanya maandalizi mapema ili kuokoa muda wa taratibu za mazishi, kuhakikisha kuwa na cheti cha kifo kuondoa usumbufu wa kuchukua mwili wa marehemu kutoka chumba cha kuhifadhia maiti na mengine.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani aliwatia moyo wanafamilia kuwa na moyo wa ustahimilivu katika wakati huo mgumu wa majonzi.
Marehemu Naitovuaki alizaliwa tarehe 15 Aprili, 1944 na kufikwa na umauti tarehe 29 Septemba, 2024. Ameacha watoto tisa (9), wajukuu 26 na vitukuu 13.
Mahakama ya Tanzania inaungana na ndugu, jamaa na marafiki kuomboleza msiba huo mzito. Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe.
Watumishi wa Mungu wakiongozwa na Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Magharibi Kati Tabora, Dkt. Kisiri Laizer (katikati) wakiwa katika ibada ya mazishi ya marehemu Naitovuaki Mosses Lengutai aliyekuwa Mama mzazi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salumu akitoa salaam za pole kwa familia ya marehemu Naitovuaki Mosses Lengutai.
Waombolezaji
Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika eneo la makaburi ambapo Mama mzazi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama alipozikwa leo tarehe 05 Oktoba, 2024 jijini Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni