Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Mahakama Sports Club imezoa jumla ya vikombe vya ushindi vitano kwa mpigo katika kilele cha mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yaliyohitimishwa tarehe 5 Oktoba, 2024 katika uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro.
Vikombe hivyo vilitolewa na mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene mbele ya viongozi mbalimbali huku upande wa Mahakama Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akiwepo jukwaani kushuhudia namna ambavyo Mahakama inabeba vikombe hivyo vya ushindi.
Mahakama Sports imebeba kikombe cha mshindi wa pili kwenye mchezo wa Kamba Wanaume ambayo ilikuwa ikivutana na Ikulu wakati upande wa Wanawake ikichukua kikombe cha mshindi wa tatu baada ya kuwabwaga Mashtaka, vikombe hivyo viliambatana na medali kwa kila mshiriki.
Kwenye mchezo wa riadha kwa ujumla Mahakama ilinyakua kikombe cha mshindi wa pili ikiwakilishwa na mfukuza upepo wa mbio ndefu Juster Tibendelana ambaye pia ni mshindi wa kwanza upande wa wanawake katika mbio za mita elfu tatu, elfu moja na mia tano pamoja na mbio za mita mia nane.
Aidha, kwa upande wa mchezo wa bao Mahakama imeendelea kuitetea nafasi yake kwa kutwaa kikombe cha mshindi wa kwanza upande wa Wanaume ikiwakilishwa na mchezaji Hashimu Rashid wakati kwa upande wa wanawake Filomena Haule aliipatia Mahakama ports sifa ya kunyakua kombe la mshindi wa pili na kupelekea idadi ya vikombe kutimia vitano.
Baada ya zoezi la kukabidhiwa vikombe likafuatia zoezi la kutunikiwa medali mbalimbali za ushindi ambapo washiriki toka Mahakama hawakutulia kwenye viti vyao kutokana na kunyanyuliwa kila wakati kwenda jukwaa kuu ili waweze kuvalishwa medali mbalimbali za ushindi katika michezo iliyoshiriki.
Akizungumza mara baada ya mashindano hayo ya SHIMIWI yaliyoanza rasmi mnamo tarehe 18 Septemba 2024, Katibu wa klabu hiyo, Dornald Tende alisema kuwa Mahakama Sports Club ilishiriki katika michezo ya Kamba, Riadha, Bao, karata na tufe ambayo iliishia hatua ya makundi, mpira wa miguu ambayo Mahakama iliishia hatua ya robo fainali wakati upande wa mpira wa pete Mahakama iliishia hatua ya kumi na sita bora.
“Vikombe hivi ni zawadi kwa muajiri wetu kwa kuthamini na kuona umuhimu wa sisi kuiwakilisha Mahakama kwenye michezo hii muhimu, tunaahidi kujipanga vyema katika mashindano yajayo,” alihitimisha Tende.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (aliyeinua kombe juu), viongozi wa Mahakama Kanda ya Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji toka Mahakama Sports wakisherekea zawadi ya vikombe vya ushindi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akifurahia vikombe vya ushindi pamoja na wachezaji toka Mahakama Sports Club.
Furaha ya kunyakua vikombe vingi vya ubingwa.
Nahodha wa timu ya kamba wanawake toka Mahakama Sports akipokea kikombe cha mshindi wa tatu wa mchezo huo toka kwa mgeni rasmi, Mhe. George Simbachawene.
Nahodha wa timu ya kamba wanaume toka Mahakama Sports akipokea kikombe cha mshindi wa pili katika mchezo huo.
Mfukuza upepo wa masafa marefu toka Mahakama Sports Juster Tibendelana akipokea kikombe cha ushindi toka kwa mgeni rasmi.
Mshindi wa pili wa bao wanawake Filomena Haule toka Mahakama Sports akipokea zawadi ya kikombe toka kwa mgeni rasmi.
Mshindi wa kwanza wa mchezo wa bao wanaume Hashimu Rashid akipokea kikombe cha ushindi toka kwa mgeni rasmi.
Baadhi wa wanamichezo toka Mahakama Sports wakionesha medali mbalimbali za ushindi walizovalishwa katika kilele cha michezo ya SHIMIWI.
Wanamichezo toka Mahakama Sports wakiingia uwanjani kwa maandamano katika kilele cha Michezo ya SHIMIWI mkoani Morogoro kwa mwaka 2024.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni