Na Daniel Sichula – Mahakama Mbeya
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles
Tiganga amezindua hudumu ya Mahakama Inayotembea jijini Mbeya na kusema kuwa,
Mahakama hiyo itaanza kufanya kazi mapema mwezi Oktoba, 2024 kwa kutoa huduma
ya kuendesha mashauri katika Kata nne za Utengule, Usongwe, Iganzo na Ilemi zilizopo
jijini hapo.
Akizungumza
hivi karibuni wakati wa hafla na zoezi la uzinduzi huo uliofanyika katika
viwanja vya Standi ya Mbalizi jijini hapo Mhe. Tiganga alisema, Mahakama ya Tanzania
inao mpango wa kusogeza huduma za kimahakama katika kila Kata. Hivyo kabla mpango
wa utekelezaji wa ujenzi wa Mahakama hizo haujaanza, Mbeya imekua moja kati ya
mikoa mitano nchini iliyopatiwa gari maalum la Mahakama Inayotembea ili kusogeza
na kutoa huduma za kimahakama karibu zaidi na wananchi waliombali na huduma
hizo.
“Napenda
kuchukua fursa hii kuwatoa hofu wananchi na wakazi wa jiji la Mbeya na viunga
vyake kuwa, huduma za kimahakama zitakazotolewa kwenye hili gari maalum la
Mahakama Inayotembea ni sawa kabisa na huduma zinazotolewa kwenye majengo ya Mahakama
za kawaida,” alisisitiza Jaji Tiganga.
Wakati
huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi Homera, aliipongeza Mahakama Kuu,
Kanda ya Mbeya kwa jitihada hizo za kutanua wigo wa kutoa huduma za haki ili
kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa haraka na kwa wakati. Utoaji huu wa huduma ya
haki kwa wananchi utakao zingatia msingi wa kufuata sheria ikiwa ni njia moja wapo
ya kusogeza huduma za kimahakama karibu zaidi na wananchi ni ya kupongezwa na
kila mpenda maendeleo kwa wakazi wa Mbeya.
Naye,
Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini Mhe. Oran Njeza aliipongeza Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Mbeya kwa hatua waliochukua ya kuweza kuwafikishia wananchi huduma
za kimahakama hasa katika maeneo ambayo yako mbali na huduma za kimahakama.
Nao
baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla ya uziduzi wa gari hilo maalum la
Mahakama Inayotembea waliipongeza Mahakama na kusema kuwa Mahakama imejidhatiti
kuhakikisha hakuna mwananchi wa kawaida atakaye shindwa kufika mahakamani
kupata huduma ya haki katika mazingira yoyote kwani sasa watafikiwa kirahisi
zaidi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga akitoa hotuba ya uzinduzi wa gari Maalum litakalo tumika kutoa hudumu ya Mahakama Inayotembea jijini Mbeya katika hafla iliyofanyika viwanja vya standi ya mabasi ya Mbalizi jijini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi Homera akifafanua jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa gari maalum la Mahakama Inayotembea.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga akiwa pamoja na viongozi waandamizi walioshiriki hafla hiyo wakiwa tayari kufanya ukaguzi wa Mahakama hiyo Inayotembea mara baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali walioshiriki hafla hiyo.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi mbalimbali wa Mahakama walioshiriki hafla hiyo.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni