Jumatano, 16 Oktoba 2024

JAJI NDIKA AFUNGUA WARSHA KUHUSU MAKOSA YA UJANGILI NA ULINZI WA MALIASILI

Na: INNOCENT KANSHA NA SALUM TAWANI-Mahakama

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt.  Gerald Ndika leo tarehe 16 Oktoba, 2024 amefungua warsha ya kikanda ya wadau wa haki jinai kutoka Malawi, Tanzania na Zimbabwe kuhusu biashara haramu ya wanyamapori katika Hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam.

Warsha hiyo imehudhuriwa na Maafisa wa Mahakama, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Waendesha Mashtaka, Wapepelezi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kutoka Tanzania, Malawi na Zimbabwe, ikiwa ni baada ya hitimisho la mafunzo ya mfululizo ya kina kuhusu uendeshaji wa mashauri ya wanyapori na misitu yaliyoendeshwa katika nchi hizo tatu.

“Mafunzo hayo yaliyofanyika yameweka msingi wa warsha hii ya kikanda na kwa kuzingatia mafanikio ya mafunzo, washiriki wa warsha hii watajadiliana mambo mengi yanayolenga kuimarisha uwezo wao wa kuvunja mitandao ya biashara haramu ya wanyamapori na kuboresha mifumo ya sheria ya ulinzi wa wanyamapori. Washiriki watapata pia fursa ya kuanzisha ushirikiano mpya na kuimarisha mitandao iliyopo ili kuratibu juhudi za kulinda urithi wa wanyamapori wa Afrika…

 “Ni hatua muhimu katika juhudi zetu za pamoja za kupambana na biashara haramu ya wanyamapori, kwa kufanya kazi pamoja tukivuka mipaka, tunaweza kulinda wanyamapori wetu, jamii zetu, na rasilimali zetu za asili kwa ufanisi zaidi. amesema Mhe.  Ndika.

Jaji Ndika ameendelea kusema kuwa kupitia warsha hiyo kutaimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo tatu katika kukomesha biashara haramu ya wanyamapori, kubadilishana uzoefu katika namna bora ya kukabiliana na makosa ya ujangili na ulinzi wa maliasili na kujadiliana jinsi ya kutatua changamoto ya biashara hiyo.

 Aidha amefafanua kuwa biashara hiyo ina athari kubwa kwenye jamii zetu inaharibu mfumo mzima wa uzalishaji viumbe hai pamoja na mazingira yao, kwahiyo warsha hiyo itasaidia kujadili kwa pamoja namna bora ya kudhibiti  mtandao unaohusika na suala hilo. 

“Makosa haya ya uhalifu yanadhoofisha utunzaji wa maliasili zetu, usalama wa Taifa pamoja na uimara wa uchumi katika jamii zetu, kwa nchi kama Tanzania, Zimbabwe pamoja na Malawi utalii ni chombo muhimu cha kuingiza mapato ya Taifa kupotea kwao inamaanisha kutaiingiza nchi hasara katika kujiingizia pato la Taifa na kusababisha kudhoofisha maendeleo ya jamii,” amesisitiza.

Ameongeza kwamba kupambana na biashara haramu ya wanyamapori sio tu suala la kimazingira, bali pia ni la kiuchumi, hivyo basi ukomeshaji wa biashara hiyo haramu ni jambo linalopaswa kutiliwa mkazo katika jamii zetu.,

Jaji Ndika amesema kuwa ukomeshwaji wa biashara hiyo haramu unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya mataifa na taasisi, hakuna Taifa linaloweza kushinda vita hiyo, ikiwa linapambana lenyewe, wawindaji haramu ni ngumu kuwakamata ila kwa ushirikiana katika nyanja zote iwe kitaifa ama kitaasisi na kuimarisha ulinzi katika mipaka husika. 

Amesema zoezi hilo litakuwa na urahisi na hatimaye kuwakamata wawindaji hawa haramu ambao wanaharibu maliasili hizo, sheria za nchi hizo zihusishe namna bora ambayo zitawabana wawindaji haramu wa maliasili zetu na hivyo ziwe kikwazo kwao katika kutekeleza azma yao ya biashara hiyo.

‘’Warsha hii itatumika kama jukwaa muhimu kwa wadau kubadilishana maarifa, uzoefu hasa katika maeneo yenye teknolojia ya hali ya juu katika kuwalinda wanyamapori,” amesema.

Jaji Ndika amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la umuhimu wa teknolojia  katika kurahisisha ukomeshaji wa  makosa hayo  ya kihalifu ya wanyamapori. Hivyo wawindaji haramu wanatumia teknolojia ya kisasa na mbinu za kufanya  makosa hayo.

 ‘’Teknolojia imekuwa ni chombo muhimu kwa Mahakama, waendesha mashtaka , na wadau wanaojihusisha uwindaji haramu,wadau wanapaswa kuimarisha matumizi ya teknolojia ili kuwa mbele ya wawindaji hao haramu,” amesema.

Jaji Ndika amekipongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kwa kuandaa semina na warsha za kujenga uwezo kwa watendaji wa makosa ya jinai inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza katika kitengo cha Mazingira, chakula na mambo ya vijijini (DEFRA) kwa kupitia Mfuko wa PAMS.

Naye Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto   Mhe. Paul Kihwelo, amesema warsha hiyo itasaidia kuleta ushirikiano miongoni wa nchi hizo tatu ili kuimarisha zoezi zima la kukomesha biashara hiyo na mtandao wa wale wote wanaojihusisha.

Ameupongeza Mfuko wa PAMS kwa kuwasaidia katika kuendesha warsha hizo kwa takribani miaka mitatu. Huku akisema sasa wapo katika nia nzuri ya kushirikiana na mataifa mengine ili kukomesha biashara hiyo.

Jaji Kihwelo amesema ni wakati mzuri kwa Mahakama, waendesha mashtaka , na wadau wanaojihusisha uwindaji haramu kukaa pamoja ili kujadiliana na kuona namna bora ya kuboresha sheria na kanuni ambazo zitakazosaidia kuwabana wale wote wanaojihusisha na uwindaji haramu wa wanyamapori

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.  Dkt. Gerald Ndika  akifungua wa warsha ya siku mbili ya kikanda  kuhusu makosa ya ujangili na ulinzi wa maliasili inayofanyika katika hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi (IJA) Lushoto  akizungumza jambo katika ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya kikanda  kuhusu makosa ya ujangili na ulinzi wa maliasili inayofanyika katika hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam.

Hakimu Mkazi Mkuu na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama(IJA)Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akizungumza jambo katika ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya kikanda  kuhusu makosa ya ujangili na ulinzi wa maliasili inayofanyika katika hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi wa Mfuko wa PAMS, Samson Kasala akizungumza jambo katika ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya kikanda  kuhusu makosa ya ujangili na ulinzi wa maliasili inayofanyika katika hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki wa warsha hiyo wakisikiliza kwa makini majadiliano kuhusu makosa ya ujangili na ulinzi wa maliasili inayofanyika katika hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam.
 Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.  Dkt. Gerald Ndika (wa kwanza kulia )na (katikati )ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye ni  Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto wakiwa katika  ufunguzi wa  warsha hiyo inayohusu makosa ya ujangili na ulinzi wa maliasili inayofanyika katika hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki wa warsha hiyo wakisikiliza kwa makini hoja zilizokuwa zikijadiliwa.
Washiriki wa warsha hiyo wakiwa katika picha ya pamoja kwenye hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.  Dkt. Gerald Ndika (aliyekaa katikati )na (kushoto wa kwanza aliyekaa) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani  Tanzania, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto Mhe. Dkt.Paul Kihwelo wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka Malawi kwenye ufunguzi wa warsha hiyo.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania,Mhe.  Dkt. Gerald Ndika (aliyekaa katikati) na (kushoto wa kwanza aliyekaa) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto Mhe. Dkt.Paul Kihwelo wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka Tanzania kwenye ufunguzi wa warsha hiyo.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.  Dkt. Gerald Ndika (aliyekaa katikati) na (kushoto wa kwanza aliyekaa) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto Mhe. Dkt. Paul Kihwelo wakiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti kwenye ufunguzi wa warsha hiyo.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.  Dkt. Gerald Ndika (aliyekaa katikati )na (kushoto wa kwanza aliyekaa) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani  Tanzania, ambaye  ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto Mhe. Dkt.Paul Kihwelo wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka  Zimbabwe kwenye  ufunguzi wa warsha hiyo.

(Picha na Innocent   Kansha- Mahakama)  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni