Na UPENDO NGITIRI- Mahakama ya Tanzania, Uswisi
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, tarehe 08 October, 2024 alitembelea Divisheni za Shirika la Miliki Bunifu (WIPO) kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya Shirika hilo na Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Nkya alipata fursa ya kufahamiana na Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Divisheni hizo, ikiwemo WIPO Judicial Institute, Kituo cha Usuluhishi na Upatanishi WIPO (WIPO Arbitration and Mediation Centre na “WIPO Academy.”
Akiwa “WIPO Judicial Institute” Msajili Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Bi. Min Eu Joo na Mwanasheria, Bi. Ines Fernandez. Mhe. Nkya aliwashukuru kwa shughuli mbalimbali ambazo zimefanywa na WIPO Judicial Institute kwa kushirikina na Mahakama ya Tanzania tangu WIPO iliposaini hati ya makubaliano na Mahakama ya Tanzania.
Aliwashukuru pia kwa kuimarisha uwezo wa kimahakama katika eneo la miliki bunifu na juhudi endelevu za ushirikiano ambazo zimekuwa na manufaa makubwa katika kuongeza ufanisi kwenye ushughulikiaji wa migogoro ya miliki bunifu Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo alishukuru kwa kazi kubwa iliyofanywa na Mahakama ya Tanzania na ushirikinao mkubwa uliopo. Aliongeza kuwa, wamekuwa wakitolea Mahakama ya Tanzania mfano kila mwaka katika Jukwaa la Majaji kwa kuwa imefanya kazi kubwa na wao wanapenda Nchi zingine wafanye vizuri kama Tanzania inavyofanya.
Katika kikao hicho, pande zote mbili zilijadili mipango ya mwakani, ikiwemo kufanya mafunzo ya ana kwa ana, kukamilisha awamu ya pili ya miongozo ya kufundishia (IP Training Materials), uhuishwaji wa maamuzi ya Mahakama ya Tanzania katika WIPO Lex na kukamilisha maandalizi ya “IP Bench book.”
Akiwa WIPO Academy, Msajili Mkuu alipokea taarifa fupi ya ushiriki wa Mahakama ya Tanzania kwenye masomo ya masafa marefu ya miliki bunifu maaalum kwa Majaji (General Distance Learning Course on IP for Judges) ambayo Majaji na Mahakimu walianza kusoma tangu mwaka 2021.
Katika taarifa hiyo, Msajili Mkuu alijulishwa kuwa Tanzania inafanya vizuri na mpaka mwaka huu wa 2024 jumla ya Majaji na Mahakimu 402 wameshanufaika na kozi hiyo. Mhe. Nkya aliwashukuru WIPO Academy kwa mafanikio hayo makubwa na kuwahidi kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kushirikiana nao kwa karibu.
Kufuatia majadiliano yaliyofanyika, mbali na Mahakama ya Tanzania kunufaika na kozi maalum ya Majaji inayotolewa kwa njia ya masafa marefu, WIPO Academy kwa kushirikiana na Mahakama itakamilisha maandalizi ya kozi mahsusi kwa Majaji na Mahakimu wa Tanzania (Customized IP course for Tanzanian Judges) pamoja na kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili miongozo ya kufundishia kozi hiyo.
Mbali na kukutana na “WIPO Judicial Institute” na “WIPO Academy”, Msajili Mkuu alipata pia fursa ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Usuluhishi, Bi. Heike Wollgast. Katika kikao hicho, Mhe. Nkya alishukuru Kituo cha Usuluhishi cha WIPO kwa kushirikiaana na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi katika kuboresha usuluhishi wa migogoro kupitia utoaji wa mafunzo juu ya usuluhishi na huduma za usuluhishi kwa njia ya mtandao. Msajili Mkuu aliwashukuru pia kwa kuwateua Majaji nane wa Tanzania kuwa Wasuluhishi wa WIPO.
Baada ya kufanyika kwa vikao hiyo kati ya Msajili Mkuu, Afisa Kiungo baina ya Mahakama ya Tanzania na WIPO na Viongozi hao wa Divisheni za WIPO, ujumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulishiriki kwenye Jukwaa la Majaji la WIPO. Jukwa hilo lilifanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 09 Oktoba, 2024 na lilihudhuriwa na Majaji zaidi ya 350 kutoka Nchi mbalimbali duniani.
Viongozi kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioshiriki jukwaa hilo katika Makao Makuu ya WIPO nchini Uswisi ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani.
Washiriki wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Aisha Ally Sinda, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Mrajisi wa Mahkama Zanzibar, Mhe. Valentine Katema, Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe. Aidan Mwilapwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzanian na Afisa Kiungo baina ya Mahakama ya Tanzania na WIPO, Mhe. Upendo Ngitiri.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (kushoto akiwa na Mkuu wa Idara ya Usuluhishi, Kituo cha Usuluhishi na Upatanishi cha WIPO, Bi. Heike Wollgast.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (kushoto) na Afisa Kiungo baina ya Mahakama na WIPO, Mhe. Upendo Ngitiri.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni