Na AMANI MTINANGI, Mahakama - Tabora
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria wa Kujitegemea Mkoa wa Tabora imeandaa mafunzo kuhusu Sheria ya Mtandao na Akili Mnemba kwa Mawakili wa Kujitegemea na baadhi ya Mahakimu wa Kanda hiyo.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Tabora, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi alisema kuwa, katika maisha ya sasa shughuli nyingi kibinadamu zimeunganishwa na mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) sambamba na Akili Mnemba.
“Ninatambua kuwa siku hizi maisha ya sasa shughuli nyingi kibinadamu zimeunganishwa na mifumo ya TEHAMA na Akili Mnemba hivyo ni jukumu letu kama wanasheria kujua njia sahihi za kushughulika na mashauri na masuala yanahusisha akili mnemba na uwasilishaji wa vidhibiti vya kielekroniki mahakamani,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.
Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza kuwa, ni muhimu na ni jukumu la Wanasheria kufahamu njia sahihi za kushughulikia mashauri na masuala yanayohusisha akili mnemba pamoja na uwasilishaji wa vidhibiti vya kielekroniki pale vinapohitajika mahakamani.
Wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Wakili Kelvin Kayaga kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Tabora, alisema Chama hicho kimeandaa mafunzo jumuishi kwa ajili ya Mawakili na Mahakimu wa Kanda ya Tabora kwa lengo la kuongeza ujuzi na maarifa ya Mawakili katika eneo la ushahidi wa kimtandao na akili mnemba.
“Tunafurahi kuandaa mafunzo jumuishi ambapo washiriki wake ni Mawakili wa Kujitegemea na Mahakimu wa Kanda ya Tabora, tukilenga kuongeza ujuzi na maarifa ya Mawakili katika eneo la ushahidi wa kimtandao na akili mnemba,” alisema Wakili Kayaga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni