Jumatano, 16 Oktoba 2024

JAJI MKUU ZANZIBAR, JAJI KIONGOZI MAHAKAMA KUU WASHIRIKI JUKWAA LA KIMATAIFA WIPO

Na Upendo Ngitiri-Mahakama ya Tanzania, Uswisi, Geneva 

 

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani hivi karibuni walishiriki kwenye Jukwaa la Majaji nchini Uswisi - Geneva kujadili mambo mbalimbali, ikiwemo Miliki Bunifu (Intellectual Property) na Akili Mnemba (Artificial Intelligence).

 

Jukwa hilo lilifanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Miliki Bunifu “World Intellectual Property Organization” (WIPO) kwa siku mbili kuanzia tarehe 09 Oktoba, 2024. Mbali na kushiriki katika Jukwaa hilo, Viongozi hao walifanya pia mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa WIPO, Bw. Daren Tang na Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WIPO, Dr. Aleman Marco.

 

Wajumbe wengine kutoka Tanzania walioshiriki Jukwaa hilo ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Aisha Ally Sinda, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Mrajisi wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe. Valentine Katema Naibu Msajili na Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe. Aidan Mwilapwa na Naibu Msajili na Mratibu wa Masuala ya Miliki Bunifu wa Mahakama ya Tanzania, Upendo Ngitiri.  

 

Jukwaa hilo lilihudhuria na Majaji  zaidi ya 350 kutoka Nchi mbalimbali duniani na dhumuni lake lililenga kubadilishana uzoefu  wa namna bora ya kushughulikia mashauri yanayohusu miliki bunifu.

 

Ushiriki wa Mahakama katika jukwaa hilo ni sehemu ya utekelezaji wa hati ya makubaliano baina ya Mahakama ya Tanzania na WIPO iliyosainiwa mwaka 2021 na utekelazaji wa ahadi wa ushirikishwaji wa Zanzibar katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na WIPO kwa kushirikina na Mahakama ya Tanzania. 

 

Itakumbukwa mwezi Novemba, 2023 alipofanya ziara ya kikazi WIPO, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliaomba katika hotuba yake Mahakama ya Zanzibar ishirikishwe kwenye shughuli mbalimbali za WIPO kwa lengo la kuboresha utoaji haki katika eneo la miliki bunifu. 

 

Katika kutekeleza ahadi hiyo, Jaji Mkuu wa Zanzibar na Mrajisi wa Mahkama Zanzibar walipata fursa ya kushiriki jukwaa hilo na kukutana pia na viongozi wa juu wa WIPO. 

 

Wakati wa Jukwaa hilo, Majaji walipata fursa ya kujadili mada mbalimbali   ikiwemo; Akili Mnemba (Artificial Intelligence); Hati Miliki; Alama za Biashara, (Trademarks), Hataza (Patent), Maboresho mahakamani, na nyingine nyingi.  


Majaji kutoka Nchi mbalimbali walitoa  pia uzoefu za Nchi zao, ikiwemo uwepo  wa Mahakama maalum ya kutatua migogoro  ya Miliki Bunifu, kutumika kwa Majaji waliobobea katika Miliki Bunifu kwenye usikilizaji wa mashauri yanayohusu miliki bunifu, uwepo wa “Technical Judges” ambao  kazi yao kubwa ni kushauri Majaji katika eneo linalohitaji  ushauri wa kitaalamu, uwepo wa kanuni  maalum  zinazotoa muongozo  na kuharakisha usikilizaji wa mashauri ya miliki bunifu.

 

Aidha, wakati wa kufanya wasilisho katika jukwaa la Majaji, Mkurugenzi wa WIPO Judicial Institute, Bi. Min Eun Joo alieleza kuwa WIPO inafanya kazi mbalimbali na Mahakama kwa dhumuni la kuziwezesha kutatua migogoro ya miliki bunifu  kwa ufanisi zaidi.

 

Mkurugenzi huyo alieleza pia kuwa WIPO imesaini Hati ya Makubaliano na Mahakama mbalimbali ikiwemo Paraquagy, Ukraine, China, Tanzania, Korea, Thailand, Misri, Albania na  Morroco.

 

 Bi. Min alitolea mfano wa Mahakama ya Tanzania na kueleza kuwa inafanya vizuri na imefanya mambo mengi kwa kushirikiana na WIPO na wangependa kufanya hivyo katika Nchi mbalimbali wanachama. Aliwaeleza Majaji walioshiriki jukwaa hilo shughuli mbalimbali zilizofanywa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na WIPO tangu mwaka 2018.

 

Mkurugenzi huyo alileza kuwa, mwaka 2019 WIPO kwa kushirikiana na  Mahakama ya Tanzania walifanya  mafunzo  ya ana  kwa ana  kwa Mahakimu jijini Dar es Salaam  na  kuanzia mwaka 2021  hadi 2024,  Majaji na Mahakimu walipata ufadhili wa kusoma  kozi maalum  ya Majaji, kozi ambayo mpaka sasa imeshawanufaisha  Majaji na Mahakimu 402 na itaendelea kutolewa kila mwaka.

 

 Aliongeza kuwa, mwaka 2021 Mahakama kwa kushirikina na WIPO waliandaa pia miongozo maalum kwa Majaji na Mahakimu ya kufundishia mada zinazohusu Miliki Bunifu na mwaka 2022 maamuzi ya Mahakama ya Tanzania na muhtasari wa maamuzi hayo yalianza kuchapishwa kwenye WIPO Lex Judgment Database, zoezi ambalo ni endelevu.

 

Alieleza vilevile kuwa, mwezi Februari, 2023 kongamano la miliki bunifu   lilifanyika kwa njia ya mtandao na Mwezi Novemba, 2023 ujumbe kutoka Mahakama ya Tanzania ulioongozwa na Jaji Kiongozi ulifanya ziara WIPO na mwezi Juni, 2024 kongamano kubwa la kimahakama kuhusu miliki bunifu   lilifanyika  Jijini Dar es Salaam. 

 

Bi.  Min aligusia pia kuwa hivi sasa WIPO kwa kushirikina na Mahakama ya Tanzania inaandaa “IP benchbook” na inatarajiwa kukamilika mwaka 2025.


Mbali na kushiriki jukwaa hilo wakiwa Geneva, Jaji Mkuu wa Zanzibar na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wajumbe waliombatana nao, walipata fursa ya kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa WIPO, Bw.  Daren Tang ambaye alieleza furaha yake juu ya ushirikiano baina ya Mahakama ya Tanzania na WIPO na kupongeza kazi kubwa iliyofanywa na  Mahakama ya Tanzania  kwa kushirikiana na WIPO katika eneo la miliki bunifu. 

 

Daren Tang alieleza kuwa tangu Mahakama ya Tanzania iliposaini hati ya makubalino na WIPO   milango ya Mahakama za Nchi zingine kusaini hati ya makubaliano na WIPO ilifunguka 

 

Naye Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WIPO, Dkt. Aleman Marco, alipokutana na ujumbe huo katika kikao maalum kilichoandaliwa kwa dhumuni la kuwasilisha salaam za Jaji Mkuu wa Tanzania na kuwatambulisha rasmi Jaji Mkuu wa Zanzibar na wajumbe wengine waliongozana na viongozi hao, aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kushiriki katika jukwaa hilo na kwa  kazi mbalimbali zilizofanywa  na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikina na WIPO.   

 

Dkt. Aleman alieleza pia kuwa, tangu Mahakama iliposaini Hati ya Makubalino     zimefanyika shughuli mbalimbali kwa kushirikiana na WIPO lakini bado wanapenda kusikia kutoka Mahakama ya Tanzania ni mambo gani mengine  wanapenda  kufanyiwa na WIPO.

 

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi baada ya kumtambulisha Jaji Mkuu wa Zanzibar na wajumbe alioambatana nao, alifikisha salamu na shukrani kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania.  Jaji Kiongozi   aliwashukuru WIPO kwa mchango mkubwa kwa Mahakama na majadiliano yenye tija yaliyofanyika baina ya Msajili Mkuu, Afisa Kiungo baina ya Mahakama na WIPO na Divisheni mbalimbali za WIPO siku ya tarehe 08 Oktoba, 2024.  

 

Baada ya Mkutano huo kukamilika, Viongozi hao walitembelea Ubalozi wa Tanzania Geneva siku ya tarehe 11 Oktoba, 2024 ambapo walifanya mazungumzo na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, Uswiswi, Mhe.  Dkt. Abdallah Possi.  Aidha, viongozi hao walimshukuru Balozi kwa ushirikiano mkubwa aliouonesha kwa kipindi chote walipokuwa Geneva na kwa ukarimu wake. 

 

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (wa kwanza kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirikika la Miliki Bunifu, "WIPO” Bw. Daren Tang (katikati) na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirikika la Miliki Bunifu, “WIPO” Bw. Daren Tang (wa nne kutoka kushoto),wa nne  kulia ni Jaji Kiongozi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, wa tatu kutoka kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, wa kwanza kutoka kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Aisha Sinda, wa pili kutoka kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, wa kwanza kushoto ni Mrajisi wa Mahkama Zanzibar, Mhe. Valentine Katema na wa pili kutoka kushoto ni Naibu Msajili na Mratibu wa Masuala ya Miliki Bunifu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri.

Washiriki kutoka nchi mbalimbali duniani waliohudhuria Jukwaa la Miliki Bunifu la Majaji. 


 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa pili kutoka kulia) akibadhi zawadi kwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WIPO, Dkt. Aleman Marco.



Mkurugenzi Mkuu wa Shirikika la Miliki Bunifu, “WIPO” Bw. Daren Tang (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili na Mratibu wa Masuala ya Miliki Bunifu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri.


Picha ya pamoja ikiwajumuisha Balozi Dkt. Abdalla Possi (wa nne kutoka kulia), wa nne kutoka kushoto ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, wa tatu kutoka kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, wa   tatu kutoka kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Aisha Sinda, wa pili kutoka kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, wa pili kutoka kushoto ni Mrajisi wa Mahkama Zanzibar, Mhe.Valentine Katema, wa kwanza kutoka kushoto ni Naibu Msajili, Mhe. Aidan Mwilapwa na   wa kwanza kulia ni Naibu Msajili na Mratibu wa Masuala ya Miliki Bunifu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri.


(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni