Na NOEL SYLIVESTER – Mahakama, Songea
Kufuatia uchaguzi wa Serikari za Mitaa mwezi Novemba 2024, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, imetoa mafunzo ya uchaguzi kwa Mahakimu katika Kanda hiyo ili kuwajengea uelewa wa masuala mbalimbali, ikiwemo sheria zinazotumika kwenye zoezi hilo.
Mafunzo hayo yalifanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Huntlcub Ruhuwiko mjini Songea na kufunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Songea Mhe. James Karayemaha.
Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Jaji Karayemaha alisema mafunzo hayo yameandaliwa kama sehemu ya utekelezaji wa sera ya mafunzo ya mwaka 2019 ambayo yatawajengea uwezo Mahakimu kufahamu sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024.
“Mafunzo haya yatawasaidia washiriki kujua sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza uchaguzi, yatasaidia kujua namna bora ya kupokea, kusikiliza na kuamua migogoro ya aina yoyote itakayoletwa mbele yao,” alisema.
Jaji Mfawidhi alieleza kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu katika suala zima la kidemokrasia nchini ambapo Mahakimu wote wa Tanzania ni sehemu ya mchakato wa kufanikisha uchaguzi huo kama Makamishina wa Viapo.
Alisema kuwa Mahakimu kuwa ndiyo watakaowaapisha Wasimamizi wa Uchaguzi na Viongozi watakaochaguliwa kabla ya kuanza kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Mwezeshaji wa Mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mhe. Japhet Manyama amemshukuru na kumpongeza Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Emmanuel Kawishe kwa kuendesha mafunzo hayo.
“Mafunzo haya yanatolewa kwa Mahakimu kwa lengo la kuwaandaa kwa ajili ya kusikiliza na kuamua mashauri yatakayotokea wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Songea Mhe. James Karayemaha (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Emmanuel Kawishe (wa kwanza kushoto) na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mhe. Japhet Manyama.
Picha ya pamoja kwa waliohudhuria mafunzo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni