• Wafurahishwa na muda mfupi unaotumika katika usikilizwaji wa mashauri katika Mahakama hiyo
Na NAOMI KITONKA, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke
Washirika wa huduma ya ulinzi wa mtoto kutoka Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wakiongozwa na Mkurugenzi wa Kimataifa wa Ulinzi wa Watoto, Bi. Sheema Sen Gupta wametembelea Mahakama ya Watoto iliyopo kwenye Kituo Jumuishi cha Masuala ya Ndoa na Familia Temeke lengo likiwa ni kufahamu huduma zinazotolewa na kupatikana katika Mahakama hiyo.
Wakiongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu katika kituo hicho Mhe. Frank Moshi kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, Mtendaji wa Kituo Jumuishi hicho, Bw. Samson Mashalla pamoja na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto katika Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Mwamini Kazema, wageni hao walipata nafasi ya kufanya ziara katika jengo la Mahakama ya Watoto na kupata fursa ya kuona jinsi Mahakama hiyo inavyofanya kazi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Frank Moshi aliwakaribisha na kusema, “tunafurahia uwepo wenu mahali hapa, ninyi mmekuwa wadau wakubwa katika kuhakikisha mazingira ya ulinzi kwa watoto na vijana ikiwemo kuhakikisha wanapata huduma bora katika maendeleo na pia kibinadamu hivyo tunawakaribisha muone huduma zetu katika Mahakama ya Watoto.”
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto, Mhe. Mwamini Kazema aliwatembeza wageni katika maeneo mbalimbali ya Mahakama hiyo na katika ofisi za wadau wake kutoka Ustawi wa Jamii na Msaada wa Kisheria huku akitoa shukrani za dhati kwa UNICEF kwa kuchangia maendeleo ya Huduma kwa Watoto.
“Kwa sasa huduma za usikilizwaji wa mashauri katika Mahakama yetu umeboreshwa sana, tunawashukuru UNICEF kwa kutusaidia kupata vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambavyo vinatusaidia katika usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao yaani ‘Virtual Court’ ambapo hali hii inawapa wananchi fursa ya kupata huduma za kimahakama mahali popote walipo kwa njia ya mtandao na pia kupunguza athari za kuonana au kuwa sehemu moja kati ya Manusura na Mtuhumiwa wakati wa usikilizwaji wa mashauri pamoja na kusaidia kwenda na muda katika kusaidia upatikanaji haki,” alisema Mhe. Kazema.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto, Bi. Asha Ally Mbaruku alitoa ufafanuzi akisema, mpaka sasa, Ofisi ya Ustawi wa Jamii inatoa huduma za kuandaa ripoti katika maombi ya ulinzi, malezi na uhalali wa uzazi.
Aidha, Afisa huyo alieleza kuwa pamoja na kuhusika katika kusikiliza na kuandaa ripoti katika mashauri ya madai Maafisa hao huhusika katika mashauri ya jinai yanayowakabili watoto, mfano; kufanya biashara mahali pasiporuhusiwa, unyanyasaji wa kijinsia uliovuka mipaka, kuingia nchini Tanzania kinyume cha sheria, unyang’anyi wa kutumia silaha, ubakaji na kadhalika.
“Katika mashauri yote hayo Maafisa Ustawi wa jamii wanafanya kazi kubwa ya kuwasaidia watoto kuwa salama kuanzia kwenye ngazi ya Vitongoji, Kata na Mtaa na kwa wateja wa moja kwa moja mahakamani wanapata huduma hizo kupitia Maafisa Ustawi wanaopatikana ndani ya Kituo Jumuishi,” alisema Bi. Aisha.
Akiwasilisha mada kuhusu mafanikio na changamoto ya Mahakama ya Watoto kwa ujumbe huo kutoka UNICEF, Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Evodia Kyaruzi alisema, “Sheria inataka kwamba shauri lililowasilishwa katika Mahakama ya Watoto lazima likamilishwe ndani ya miezi sita isipokuwa kwa hali maalum ambapo muda unaweza kuongezwa hadi miezi tisa.”
Mhe. Kyaruzi alisema, mashauri mengi yanayowasilishwa katika Mahakama hiyo huamuliwa ndani ya miezi mitatu tangu tarehe ya kufunguliwa.
“Takwimu zetu zinaonesha kuwa kwa kipindi cha kati ya Januari hadi Septemba, 2024 jumla ya mashauri ya madai 688 yaliyowasilishwa, 557 yaliamuliwa na hadi kufikia tarehe 30 Septemba mwaka huu, jumla ya mashauri 130 yalikuwa yanaendelea.” Alieleza Naibu Msajili huyo.
Aliongeza kuwa, miongoni mwa mashauri yanayosubiriwa ni mashauri matano pekee ndio yalikuwa na umri wa zaidi ya siku 90 tangu tarehe ya kufunguliwa. Na kwamba haikuwa hivyo kabla ya kutungwa kwa Sheria ya Mtoto.
“Hivi sasa watoa msaada wa kisheria ambao ni WLAC, WILDAF na LHRC wana mchango mkubwa katika kuhakikisha kwamba haki za mtoto zinalindwa kwa kutoa huduma za kisheria bila malipo kwa wale wanaohitaji huduma zao. Uwepo wa huduma za kisheria bila malipo hufanya Kituo hiki kuwa maalum na cha kipekee,” alisema Mhe. Kyaruzi.
Aidha, wageni hao walipata nafasi ya kuuliza maswali na kujadili ambapo walionesha kufurahishwa na muda mfupi uliowekwa katika usikilizwaji wa mashauri ya watoto.
“Tumefurahishwa na kushangazwa sana na muda wa usikilizwaji wa mashauri ya watoto kuwa kipindi cha miezi sita tu, hii ni mara ya kwanza kwa Nchi zote na Mahakama zote zenye kutoa huduma ya usikilizwaji wa mashauri ya aina hii, tunawapongeza sana,” Alisema Mkuu wa Ulinzi wa Watoto UNICEF, Bi. Miranda Armstrong.
Aidha, wageni hao pia walipata fursa ya kuonana na kuzungumza na wadau kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii ambapo walifurahi kufahamu namna wanavyohakikisha mtoto anapohusika katika shauri kama shahidi, manusura au mtuhumiwa lazima Afisa Ustawi wa Jamii ahusike wakati wote wa taratibu za kimahakama.
Wajumbe wengine kutoka UNICEF walioshiriki katika ziara hiyo ni pamoja na Mtaalamu wa Ulinzi wa Watoto kutoka NYHQ, Bi. Monica Darer, Mshauri wa Kikanda wa Ulinzi wa Mtoto, Bw. Nankali Maksud, Mkuu wa Ulinzi wa Mtoto UNICEF, Bi. Miranda Armstrong na Mtaalam wa Ulinzi wa Watoto, Upatikanaji wa Haki, Bi. Victoria Mgonela wakisindikizwa na Mtaalamu Mkuu wa Programu, Haki za Kibinadamu na Demokrasia kutoka Sida, Bi. Charlotte Stahil na Bi. Noella Lumbala, Meneja ‘Girl Capital Africa’, Mfuko wa Uwekezaji wa Watoto (CIFF).
Akitoa shukrani kwa ujumbe huo, Naibu Msajili wa Kituo hicho, Mhe. Frank Moshi alisema, “tunatambua mchango wenu mkubwa kama UNICEF katika kuimarisha utawala bora wa haki kwa watoto ambao kwa sehemu kubwa mmesaidia Chuo cha Uongozi wa Mahakama, kama chombo cha mafunzo kwa Mahakama ya Tanzania, katika kuandaa nyaraka za mafunzo ya Haki za watoto. Nyaraka hizo zinasaidia Maafisa wa Mahakama na Maafisa wote wanaohusika na Haki ya Watoto kutokana na kufanya makosa wanapomshughulikia mtoto.”
Alishukuru pia kwa uundaji wa mwongozo wa kawaida wa Mahakimu kuhusu jinsi ya kuendesha Mahakama ya Watoto kwakuwa husaidia Maafisa wa Mahakama kuhakikisha uendeshaji mzuri wa mashauri ya watoto yanayowakabili.
Shirika hilo la UNICEF linajitolea kuunda mazingira ya ulinzi kwa watoto na vijana, kuhakikisha wanapata huduma bora na zinazojumuisha ulinzi wa watoto katika miktadha ya maendeleo na ya kibinadamu, limekuwa msaada mkubwa na mdau maalumu wa shughuli za Mahakama hasa Mahakama ya Watoto.
Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Frank Moshi (wa tatu kushoto) akizungumza jambo wakati wa ziara ya Washirika kutoka UNICEF walipofanya ziara katika Mahakama hiyo hivi karibuni.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto Temeke, Mhe. Mwamini Kazema akitoa ufafanuzi kwa washirika wa Ulinzi wa Watoto kutoka UNICEF walipotembelea Mahakama hiyo hivi karibuni.
Mtaalamu Mkuu wa Programu, Haki za Kibinadamu na Demokrasia kutoka Sida, Bi. Charlotte Stahil akiuliza swali kwa Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Watoto, Mhe. Mwamini Kazema (hayupo katika picha) wakati akitoa maelezo walipotembelea katika Mahakama ya Watoto katika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni