Na NAOMI KITONKA, Kituo Jumuishi cha Masuala Familia- Temeke
Kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai (Bench Bar Meeting) kimeazimia kuwepo kwa kitengo kimoja katika Wizara ya Ardhi ili kushughulikia masuala ya ubadilishwaji wa majina katika Hati za umiliki wa ardhi kwa wale wanaofuatilia mirathi kwakuwa suala hilo limeonekana kuwa ni jambo linalochangia ukwamishaji wa zoezi la kufunga mirathi kwa wakati.
Akizungumza hivi karibuni wakati akifungua kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa alisema, hatua hiyo itasaidia kuepusha mianya ya rushwa na upotevu wa muda hasa pale wateja wanapokutana na watu wasiohusika wanapofuatilia masuala ya ubadilishwaji wa majina katika Hati za Umiliki na kukosa kujua hatua muhimu za kufuata ili kukamilisha jukumu hilo muhimu.
“Tumekuwa na wakati mzuri katika kikao kilichopita kama ilivyo siku ya kikao hiki ambapo tunategemea maoni kutoka kwenu wadau wetu wakubwa wa huduma za kimahakama na kutokana na utofauti wa huduma tunazozitoa kulingana na vitengo na idara, sisi kama Kituo Jumuishi tunategemea kujifunza kutoka kwenu na kuwasaidia wananchi kupata huduma kwa uhakika,” alisema Mhe. Mnyukwa.
Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo amewakumbusha wajumbe wa kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai (Bench Bar Meeting) kutoa maoni ya namna gani watashirikiana na Mahakama hiyo kuboresha huduma na kurahisisha zoezi la utoaji haki kwa wananchi.
Kikao hicho kiliambatana na uwasilishwaji wa ajenda kutoka kikao kilichopita na utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho ambapo wajumbe walipata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi ambapo hoja kubwa iliyoibuliwa katika majadiliano ilikua kuhusu ubadilishwaji wa majina katika hati za umiliki wa Ardhi kutoka majina ya marehemu kwenda kwenye majina ya warithi kwa sababu limeonekana ni jambo linalochangia ukwamishaji wa zoezi la kufunga mirathi kwa wakati.
Katika kikao yalijadiliwa masuala mbalimbali ambapo mmoja wa wajumbe wa kikao hicho alisema, Wasimamizi wa Mirathi wamekuwa wakikumbana na changamoto kubwa hususani katika zoezi la ubadilishwaji wa majina katika hati za umiliki wa ardhi kutoka majina ya marehemu kwenda kwenye majina ya warithi na kwamba, suala hilo limesababisha mashauri ya mirathi kuchukua muda mrefu kufikia miaka hadi miwili na zaidi.
“Kutokana na umuhimu wa kipengele hicho katika ufuatiliaji wa masuala ya mirathi tunashauri kuwepo kwa kitengo maalumu katika Wizara ya Ardhi na ngazi ya Manispaa kitakachohusika na usimamiaji na utoaji wa huduma za ubadilishwaji wa majina katika hati za umiliki kwa warithi ili kuwezesha na kuwahisha zoezi la utoaji haki na ufungwaji wa mashauri kwa wakati,” aliongeza mjumbe huyo.
Pamoja na hayo, changamoto kubwa ilionekana kuwa, wateja wengi wanaofuatilia masuala ya ardhi katika mirathi hukutana na watu wasio sahihi na hivyo kukwamishwa kwa kutokupata taarifa sahihi zinazohusu jambo hilo muhimu na kuishia kupoteza muda na pesa pasipo kufanikiwa.
Kikao hicho kilichowashirikisha Mahakimu na wadau mbalimbali wa Mahakama wa Kamati ya kusukuma Mashauri ya Madai kilihudhuriwa pia na Mtendaji wa Kituo hicho, Bw.Samson Mashalla, Naibu Wasajili, Mhe. Frank Moshi na Mhe. Evodia Kyaruzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya, Mhe. John Msafiri, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Alois Mwageni akiambatana na Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Watoto, Mhe. Mwamini Kazema.
Wadau waliohudhuria katika kikao hicho ni kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Msajili wa Hati, Chama Cha Mawakili Tanzania (TLS) pamoja na Ofisi ya Mtandao wa Mtoa Huduma (TANLAP).
Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Bw. Samson Mashalla akisikiliza kwa makini katika kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika hivi karibuni.
Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Frank Moshi (aliyesimama) akitoa mada katika kikao cha Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni