Jumapili, 20 Oktoba 2024

MAHAKAMA YA WILAYA KIBAHA HAINA MASHAURI YA MLUNDIKANO – MHE. LUKUMAI

Waweka mikakati ya kumaliza mashauri yanayoashiria mlundikano

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai amewapongeza wadau wa haki jinai kwa ushirikiano mzuri wanaotoa ambao umewezesha kumalizika kwa wakati na hatimaye Mahakama hiyo kutokuwa na mlundikano wa mashauri.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika tarehe 18 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Mahakama hiyo, Mhe. Lukumai alisema, kwa sasa kuna mashauri tu yanayoashiria mlundikano yaani zenye siku 150 ambayo nayo yamewekewa mkakati wa kuyamaliza kwa haraka kabla ya kuvuka miezi sita.

“Tunashukuru kwa ushirikiano mzuri wa Wadau wa haki jinai, kwa sasa mashauri ambayo yanatishia kuwa kwenye mlundikano ni yale tu yenye siku 150 inabidi tuzimalize kwa wakati kabla ya kufikisha miezi sita,” alisema Mhe. Lukumai.

Mfawidhi huyo aliongeza kwa kusema kuwa, Mahakama ya Wilaya Kibaha na Mahakama zote sita za Mwanzo hazina mlundikano wa mashauri ya jinai na madai.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mlandizi, Mhe. Joseph Luoga aliwaomba Polisi kuachana na mfumo wa zamani wa kuandika hati ya mashtaka kwa kalamu badala yake wazichape ili kuendana na wakati pamoja na teknolojia. 

“Tunawaomba wenzetu Jeshi la Polisi kuandaa hati za mashtaka kwa kuzichapa ili tuendane na mabadiliko ya teknologia maana kuna dhania (presumption) kwamba kesi inaweza kufika Mahakama ya Rufani hivyo kama zimeandikwa kwa kalamu zinaweza kufika zimefutika na hivyo kusababisha haki kutotendeka,” alisema Mhe. Luoga.

Mhe. Luoga aliwashauri Polisi kujiridhisha umri wa watuhumiwa kabla ya kuandaa hati na kama kuna mashaka kabla ya kufikisha mahakamani wajiridhishe maana kumekua na changamoto nyingi za umri kwa washtakiwa hati inatamka umri mkubwa akisomewa hati ya mashtaka anakana umri sio sahihi ni mdogo zaidi  ya ulioandikwa kwenye hati.

Aidha, katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wadau wa Haki Jinai wakiwemo Ustawi wa Jamii walizungumzia kuhusu malezi ya Watoto ambapo Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Matilda Zakaria aliwaomba wadau wa haki jinai kuwa mabalozi wazuri katika malezi ya watoto wakianzia nyumbani na hata kwenye jamii inayowazunguka kwani vitendo vya ukatili kwa watoto vinakithiri siku hadi siku. 

“Kumpatia mtoto elimu zuri mavazi na kumpa kila anachohitaji haitoshi kumfanya mtoto awe salama badala yake tuwe walezi kwa kuongea na watoto kuwauliza changamoto wanazokutana nazo wanapokuwa shule marafiki walio nao na kuchunguza mienendo mizima ya watoto wao badala ya kuwa wakali au kwa kuwa mama au baba ni Hakimu au Polisi basi na mtoto uishi nae kama Polisi na hii inawakosesha malezi na hivyo kusababisha watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili,” alisema Bi. Matilda.

Aliongeza kwa kusema wanaofanya ukatili kwa watoto ni ndugu wa karibu na familia hivyo umakini katika malezi unapaswa kuongezwa zaidi.

Kikao hicho  cha Kusukuma mashauri kiliazimia kuendelea kupanga mashauri kwa muda baada ya kufikia makubaliano baina ya pande zote mbili lakini pia kuendelea kutoa elimu ya sheria kwa wananchi wanaofika mahakamani mara moja kwa wiki.

Kikao hicho cha kusukuma mashauri ya jinai na madai hufanyika kila baada ya miezi mitatu katika Mahakama ya Wilaya na huhudhuriwa na wadau wa haki jinai lakini pia Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao cha Kusukuma Mashauri, Mhe. Emmael Lukumai (kushoto) pamoja na Katibu wa kikao hicho, Wakili wa Serikali, Bi. Gladness Mchami wakiwa katika kikao cha kusukuma mashauri ya jinai na madai kilichofanyika katika Mahakama hiyo hivi karibuni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mlandizi, Mhe. Joseph Luoga akizungumza jambo wakati wa 
Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika hivi karibuni.

Mwenyekiti wa Kikao cha Kusukuma mashauri ya madai ambaye ni Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi ya wilaya ya Kibaha Mhe. Emmael Lukumai(kushoto) na Katinu wa kikao hicho ambaye ni wakili wa kujitegemea wakili Philemon Mganga.

Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Matilda Zakaria akizungumza katika kikao hicho.

Wadau wa Haki Jinai wakimsikiliza Mwenyekiti wa kikao (aliyesimama).

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni