Na NAOMI KITONKA, Kituo Jumuishi cha Masuala Familia- Temeke
Wafanyakazi wa Vitengo mbalimbali vya Ofisi ya Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania wakiongozwa na Meneja wa Programu ya Jinsia, Bi. Oliva Kinabo wamefanya ziara ya mafunzo katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo iliyofanyika tarehe 18 Oktoba, 2024 walipokelewa na Jaji Mfawidhi Kituo hicho, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, Majaji wa Mahakama hiyo, Mhe. Asina Omari na Mhe. Sarah Mwaipopo, Naibu Wasajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Frank Moshi na Mhe. Evodia Kyaruzi, Mahakimu Wafawidhi kutoka Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Mahakama ya Watoto.
Akitoa salamu na utambulisho sambamba na utoaji wa elimu ya ndoa na mirathi kwa Ugeni huo kutoka Ofisi za Ubalozi wa Ireland Nchini Tanzania, Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa alisema Kituo hicho ni maalum kwa ajili ya kusikiliza mashauri maalum ya masuala ya familia.
“Kituo hiki ni maalumu kwa ajili ya kuhudumia watu maalumu na kusikiliza mashauri maalumu hivyo, tunawakaribisha ili kujifunza kwa pamoja namna Kituo chetu kinahudumia wananchi na usikilizwaji wa Mashauri ya Ndoa, Familia na Watoto, hivyo nanyi muwe wadau wa usambazaji wa elimu katika ubalozi wenu,” alisema Mhe. Mnyukwa.
Aidha, katika ziara hiyo wafanyakazi hao walipata nafasi ya kutembelea sehemu mbalimbali za jengo la Mahakama hiyo na kujulishwa huduma zinazotolewa kutoka Ofisi za Wadau mbalimbali wanaopatikana.
Walitembelea na kujionea Ofisi ya Jaji Mfawidhi na Vyumba vya kusikilizia Mashauri, Chumba cha Kunyonyeshea Watoto kwa kinamama wanaofika Mahakamani, Ofisi za Msaada wa Kisheria na Ofisi za Ustawi wa Jamii pamoja na kupata elimu kupitia mada zilizowasilishwa kutoka kwa Naibu Msajili, Mhe. Frank Moshi, Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Edna Mollel, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Watoto, Mhe. Veronica Mtete, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. Simon Swai na Hakimu Mkazi Temeke, Mhe. Loveness Mwakyambiki.
“Mahakama yetu inatumia mifumo katika uendeshwaji wake hasa huu wa Electronic Case Management (e-CMS) ambapo mteja anaweza kufungua shauri lake kwa njia ya mtandao, kujua shauri lake limepangwa lini na pia kuona mwenendo wa shauri unavyotengenezwa kwa Mfumo wa Unukuzi na Utafsiri (TTS) amri, pamoja na hukumu za mashauri pasipo kufika mahakamani na kuhudhuria kwa njia ya mtandao mashauri (Video conferencing),” alisema Mhe. Moshi wakati wageni hao walipotembelea moja ya Mahakama za wazi Kituoni hapo.
Aliongeza pia kwa kusema,“katika Kituo chetu tunatumia mfumo wa kusajili wateja wote wanaokuja kituoni kwa lengo la kuhudumiwa, hiyo hutusaidia kuwa na takwimu sahihi pamoja na mfumo wa matangazo kwa wateja wanapohudhuria Mahakamani unaomuwezesha mteja kusikia shauri lake likiitwa mahali popote katika jengo.”
Katika uwasilishwaji wa mada kuhusu usikilizwaji na hatua za kufungua Mashauri ya Ndoa iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Edna Mollel alisema, “Sheria ya Ndoa inazingatia vipengele mbalimbali katika kuhakikisha Wanandoa wanapata haki zao katika usikilizwaji wa mashauri ya Ndoa ikiwemo haki ya kugawana mali baada ya kuthibitishwa ndoa imevunjika kiasi cha kutokurekebishika kwenye kifungu cha Sheria ya Ndoa Sec. 66 na 107 (2)(b) na (c) pamoja na malezi ya Watoto.”
Katika wasilisho lililotolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Watoto, Mhe. Veronika Mtete alizungumzia jinsi mashauri ya Watoto yanavyoendeshwa huku akiainisha umri wa Watoto ambao unapatikana na madhara zaidi katika jamii ambapo alisema, “kama Mahakama ya Mtoto tunajitahidi kusikiliza mashauri yao kwa nguvu na umakini mkubwa ili kuhakikisha zoezi la upatikanaji haki kwa haraka linafikiwa tukizingatia Sheria na haki zote za mtoto kulingana na Kanuni ya adhabu Sura ya 16.”
Wageni hao walipata fursa ya kujifunza kuhusu umuhimu wa kufungua Mirathi na kuacha Wosia kwa ajili ya kuepusha migogoro ya kifamilia pindi wanapofariki.
“Sheria inayotumika kusikiliza mashauri ya mirathi inategemea na maisha ya mtu kipindi cha uhai wake na hii pia huamua aina ya Mahakama itakayosikiliza shauri hilo na taratibu zote za muhimu zinafuatwa kuanzia kwenye uteuzi wa msimamizi wa mirathi na mgawanyo wa mali,” alisema Mhe. Mwakyambiki.
Akiongezea kuhusu mada hiyo, kwa upande wake Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. Simon Swai alisisitiza kuhusu kuondoa hofu na woga wa kuandika wosia wakati mtu akiwa hai kwani wosia siyo uchuro na husaidia familia kuepukana na migogoro isiyo ya lazima na Mahakama kwa ujumla katika zoezi la utoaji haki.
Akitoa neno la shukrani wakati wa ziara hiyo kwa niaba ya Viongozi wa Ubalozi wa Ireland Nchini Tanzania, Meneja wa Programu ya Jinsia, Bi. Oliva Kinabo alisema, “tunawashukuru sana uongozi wa Kituo Jumuishi Temeke, tunajisikia vizuri kuona mafanikio makubwa katika zoezi zima la utoaji haki kwa wananchi na tumejifunza mengi yanayoweza kutusaidia katika masuala ya Mirathi na Ndoa na pia kama ubalozi tumekuwa tukishirikiana na Mahakama kwa ukaribu sana hatukuwahi kujua kuna Kituo kinatoa huduma nzuri namna hii na kwa viwango vikubwa vya Matumizi ya TEHAMA, kwa hili tunawapongeza sana.”
Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (katikati) akizungumza jambo na wageni kutoka Ofisi ya Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania walipofanya ziara katika Mahakama hiyo hivi karibuni. Kushoto ni Jaji wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Asina Omari na kulia ni Jaji wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Sarah Mwaipopo.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Edna Mollel (aliyesimama) aktitoa wasilisho wakati wa ziara ya wafanyakazi wa Ofisi za Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania iliyofanyika hivi karibuni kituoni hapo.
Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (aliyeti mbele) pamoja na Majaji wengine wa Kituo hicho (walioketi kushoto) wakimsikiliza kwa makini Meneja wa Programu ya Jinsia Kutoka Ofisi za Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Oliva Kinabo (aliyenyyosha mikono) alipotembelea Ofisi ya Jaji Mfawidhi wakati wa ziara Ubalozi huo iliyofanyika hivi karibuni kushoto kwake ni Mkuu wa Idara ya Fedha wa Ubalozi huo, Bw. Nilesh Shukla.
Naibu Msajili wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Frank Moshi (kulia) akitoa maelezo wakati wa ziara ya Wafanyakazi wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania iliyofanyika katika Mahakama hiyo hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni