Na Christopher Msagati- Mahakama Manyara
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. John Rugalema Kahyoza tarehe 18 Oktoba, 2024
aliwaongoza Watumishi wa Kanda hiyo katika viwanja vya Mahakama Kuu kumpokea
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Nenelwa Joyce Mwihambi, ambaye
amepangiwa kazi katika Kituo hicho.
Akizungumza mara baada ya kumpokea
Jaji Mwihambi, Mhe. Kahyoza amemueleza kuwa, Mahakama Kuu Kanda ya Manyara
itampatia ushirikiano wa kutosha katika majukumu yake mapya na kumsaidia katika
kutimiza malengo ya Mahakama ya kumaliza mashauri ndani ya muda mfupi.
“Mahakama Kuu Kanda ya Manyara
imejiwekea malengo ya kumaliza mashauri ndani ya miezi sita na tunajitahidi
kufanya hivyo ili wananchi wapate unafuu wa kupata haki zao kwa wakati”.
Alisema Mhe. Kahyoza.
Kwa upande wake Mhe. Mwihambi
ameushukuru uongozi wa Mahakama Kanda ya Manyara ukiongozwa na Jaji Mfawidhi
kwa mapokezi mazuri waliyoyafanya katika kituo chake kipya cha kazi na kuongeza
kwamba, anaamini kuwa atajifunza mambo mengi atakapokuwa Mahakama Kuu Manyara
kwa kuwa ni kituo chake cha kwanza kufanya kazi kama Jaji.
“Manyara kwangu itakuwa ni shule ya
kujifunza vizuri shughuli hizi za ujaji kwa kuwa ndiyo kituo changu cha kwanza
kuhudumu mara baada ya kuteuliwa kuwa Jaji,” amesema Jaji Mwihambi.
Mhe. Mwihambi ni Jaji mpya wa
Mahakama Kuu ya Tanzania aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Aidha kabla ya uteuzi
huo Mhe. Mwihambi alikuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ujio wa Jaji huyo utaongeza nguvu
katika usikilizwaji wa mashauri katika Kanda hiyo, hata hivyo Kanda hiyo itakuwa
na jumla ya Majaji wanne ambao wamejipanga kuhakikisha mashauri yanayosajiliwa
yanasikilizwa na kuamuliwa kwa haraka ili kuendana Dira ya Mahakama ya utoaji
wa haki sawa kwa wote na kwa wakati.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza
(Mwenye tai nyekundu) akimtambulisha Mhe. Nenelwa Mwihambi kwa Watumishi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Manyara.
Mhe.
jaji Nenelwa Mwihambi akiwa katika ofisi yake mpya mara baada ya kukaribishwa.
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (mwenye tai nyekundu)
akiwa kwenye picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda Manyara Mhe. Nenelwa
Mwihambi (wa nne kutoka kushoto), wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Manyara Mhe. Frank Mirindo, wa tano kutoka kushoto ni ambaye ni Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe Bernard Mpepo. Wengine waliosimama
mstari wa nyuma ni watumishi wa Mahakama Kanda Kuu Kanda ya Manyara.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni