Na. MUSSA MWINJUMA-Tanga
Jana tarehe 20 Oktoba, 2024, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocati Mteule aliongoza kikao cha menejimenti kilichofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Wilaya ya Korogwe, jijini hapa.
Pamoja naye alikuwepo pia Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Messe John Chaba, Naibu Msajili, Mhe. Hudi Majid Hudi, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Bi. Subira Ismail Mwishashi, pamoja na watumishi wengine ambao ni wajumbe wa kikao hicho.
Lengo la kikao hicho cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025 lilikuwa kupeana taarifa mbalimbali za kiutendaji na kiutumishi, pamoja na kujua hali ya uendeshaji wa mashauri ndani ya Kanda hiyo.
Kabla ya kikao hicho kuanza, Jaji Mfawidhi na wajumbe wengine walitembelea na kukagua ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Korogwe na kujionea maendeleo ya jengo hilo la kisasa la Mahakama ambalo,kwa mujibu wa Mkandarasi, limefikia asilimia 80 ya ujenzi wake.
Pamoja na mambo mengi yaliyoongelewa katika kikao hicho, Jaji Katarina aliwakumbusha wajumbe kuhusu umuhimu wa vikao kama hivyo kwa kuwa ni nyenzo muhimu katika utendaji kazi. “Vikao kama hivi ni muhimu hata katika sehemu zenu za kazi kwa kuwa ni nyenzo kubwa kwa ustawi wa vituo vyenu,” alisema.
Aidha, Jaji Mfawidhi alisisitiza kwa wajumbe wa mkutano huo kwamba wao kama Viongozi katika maeneo yao ya kazi ni lazima kusimamia kikamilifu maslahi ya watumishi wao, akiwaasa maafisa utumishi juu ya kuwaangalia watumishi.
“Kila mtumishi unayemuona mahakamani, ujue yupo pale ili kusaidia kesi zisikilizwe, hana kazi nyingine. Hivyo maafisa utumishi hakikisheni maslahi ya wafanyakazi hawa yanapatikana kwa wakati,” alisisitiza
Taarifa mbalimbali za mashauri ziliwasilishwa katika kikao hicho ambapo kwa baadhi ya Mahakama zilikua na kesi za mlundikano na sababu kubwa zilizotajwa ni mapingamizi ya mara kwa mara, dharura za Mawakili, upelelezi kutokamilika kwa wakati na kuchelewa kupatikana kwa mashahidi.
Mahakama za Wilaya ya Handeni, Kilindi, Mkinga na Pangani hakukuwa kesi za mlundikano, hivyo Jaji Mfawidhi alisisitiza juu ya ushirikiano na wadau ili kuweza kutatua changamoto za ucheleweshwaji wa kesi hizo kwa Mahakama zenye kesi za mlundikano ambazo ni Mahakama za Wilaya Tanga, Muheza,Korogwe na Lushoto.
Akizungumzia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Jaji Katarina alisema “Kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Mahakama katika eno hili la TEHAMA, tafadhali tusikwame katika kuendesha mashauri kwa kutumia teknolojia.”
Alitoa mfano wa Mahakama ya Wilaya Kilindi ambapo kesi 55 zilisikilizwa kwa njia ya mtandao ndani ya kipindi cha miezi mitatu, huku mahabusu wakiwa wilayani Handeni ambako kuna Gereza na Hakimu akiwa wilayani Kilindi, baaada ya Mahakama ya Tanzania kupeleka vifaa vya kisasa vya kielektroniki katika Gereza hilo.
Kabla ya kufunga kikao hicho, Jaji Mfawidhi alitoa maelekezo kwa Mahakimu Wafawidhi ambao ni wajumbe wa kikao hicho kwenda kupandisha taarifa zote zinazohusiana na mashauri kwenye mfumo wa kusajili mashauri.
“Kila mtu akachunguze na ahakikishe kila kesi iwe na kumbukumbu zote, vielelezo vyote na kama kuna taarifa zinazokosekana, basi ziwekwe kwenye kesi husika ndani ya mfumo ili taarifa ya mwisho ya kielektroniki iwe ni taarifa iliyokamilika,” alisisitiza Jaji Katarina.
Naye Mhe. Chaba, ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu ya Kanda aliwashukuru wajumbe wa Mkutano huo kwa taarifa zao, lakini pia alipongeza kuona taarifa zote zinaonesha kuna utoaji wa elimu mahala pa kazi na kwa kila Mahakama kuwa na programu maalum walizojiwekea.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocati Mteule (katikati) akiongoza kikao cha Viongozi wa Kanda wilayani korogwe, kulia kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Messe Chaba na kushoto kwake ni Naibu Msajili, Mhe. Hudi Majid Hudi.
Wajumbe kutoka Wilaya mbalimbali waliohudhuria kikao hicho ambao ni Mahakimu Wakazi Wafawidhi.
Wajumbe kutoka Mahakama Kuu Tanga waliohudhuria kikao hicho ambao ni Sekretarieti.
Wajumbe kutoka Wilaya mbalimbali waliohudhuria kikao hicho ambao ni Maafisa Utumishi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocati Mteule (alievaa suti) akipata maelezo ya Mkandarasi wa Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Korogwe, Mhandisi George Onesmo kutoka Kampuni ya Moladi Co.Ltd ambao ndio wajenzi wa jengo hilo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni