Jumanne, 22 Oktoba 2024

MAHAKIMU MBEYA WANOLEWA KUHUSU UTATUZI WA MIGOGORO ITOKANAYO NA UCHAGUZI

Na Daniel Sichula - Mahakama Mbeya

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya imeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo Mahakimu wote kutoka mikoa ya Mbeya na Songwe ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri na utatuzi wa migogoro itokanayo na uchaguzi (Elector Dispute Resolution-EDR).

Akizungumza wakati wa kufungua mafuzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya BEACO jijini Mbeya mnamo tarehe 18 Oktoba 2024 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga alisema kuwa elimu hiyo ni mwendelezo wa mafunzo ya wakufunzi katika utatuzi wa migogoro ya uchaguzi yaliyofanyika jijini Dar es salaam mnamo tarehe 17 Septemba 2024.

Mhe. Tiganga aliongeza kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwani yatawajengea uwezo Mahakimu pale watakapo kuwa wanaendesha mashauri yanayotokana na uchaguzi hasa uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa utakao fanyika mwezi Novemba 2024. Hatua hii ni muhimu kwani itasaidia wananchi kupata viongozi waliowachagua kwa kushughulikia mashauri yao kwa haraka yanapopelekwa mahakamani baada ya wananchi kutoridhishwa aidha na mchakato wa uchaguzi, uchaguzi wenyewe ama matokeo ya uchaguzi.

“Mafunzo haya yatasaidia mahakimu katika kusikiliza na kutoa hukumu za mashauri ya uchaguzi kwa wakati na kwa weledi, kwa kuwa mahakama inawajibu wa kutatua migogoro ya uchaguzi ndani ya muda mfupi pale ambapo miongoni mwa washindani hawajaridhishwa na zoezi zima la uchaguzi,” alisema Mhe. Tiganga.

Aidha, Mhe. Tiganga aliwaomba washiriki wote kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo kwa kusikiliza na kuuliza maswali ya ufafanuzi ili kujenga uwezo zaidi katika kuelewa mifumo ya usimamizi wa uchaguzi, na namna ya kutatua migogoro inapofikishwa mbele yao. Aidha amewataka kuzingatia mafunzo hayo ambayo yana husisha mada mbalimbali zikiwemo za maadili ya maafisa wa mahakama na namna bora ya uendeshaji wa mashauri na uandishi wa hukumu za mashauri ya uchaguzi yanayotokana na matukio ya kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Jaji Mfawidhi huyo, aliushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania, kwa kuruhusu mafunzo haya kufanyika, na pia aliushukuru Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ushirikiano wake na wadau wengine wakiwemo International Foundation for Electrol Systems (IFES) na USAID kuweza kuandaa mtaala wa mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi na kuwezesha mafunzo haya kufanyika.

Kwa upande wake, Naibu Msajili Mfawidhi Mhe. Aziza Temu alisema umuhimu wa mafunzo hayo kwa Maafisa Mahakama ni kuandaa utayari wa kuweza kutambua mifumo ya usimamizi wa uchaguzi, uendeshaji wa uchaguzi, uelewa kwenye migogoro ya uchaguzi pamoja utatuzi wake.

“Ni muhimu kila mmoja wetu kutenda haki, ili kujenga imani ya wananchi juu ya chombo chao utoaji haki kwa kuzingatia kwamba uchaguzi na Mahakama havitengani kwani maamuzi yanayotokana na mashauri ya uchaguzi yanawagusa wananchi moja kwa moja katika kujenga imani ya utawala wa sheria. Kwa hiyo, pamoja na kutafsri sheria kwa weledi ni muhimu pia kusimamia haki kwenye migogoro ya uchaguzi,” alisisitiza Mhe. Temu.  

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga (katikati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa mafunzo ya namna bora ya kutatua migogoro itokanayo na uchaguzi, wapili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya namna bora ya utatuzi wa migogoro itokanayo na uchaguzi katika Ukumbi wa BEACO jijini Mbeya.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa ambeye ni Mkufunzi wa Mafunzo hayo akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya namna bora ya kutatua migogoro itokanayo na uchaguzi wakifuatilia jambo kwa umakini mkubwa.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa (aliyeshika kisemeo) ambeye ni Mkufunzi wa Mafunzo hayo akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni