Jumatano, 23 Oktoba 2024

MAHAKAMA YA RUFANI KUSIKILIZA MASHAURI 50 ARUSHA

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Mahakama ya Rufani Tanzania imepiga kambi mkoani Arusha katika moja ya vikao vyake vya kusikiliza mashauri yaliyowasilishwa mbele yake ambapo katika Kikao hicho Mahakama hiyo imepanga kusikiliza jumla ya mashauri 50.

Kikao hicho maalum cha kusikiliza mashauri hayo (session) kilianza Jumatatu tarehe 21 Oktoba, 2024 katika Kituo Jumuishai cha Utoaji Haki (IJC) Arusha na kinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 08 Novemba, 2024 ambapo idadi hiyo ya mashauri ya aina mbalimbali yatasikilizwa na kuamuliwa.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Wanjah Hamza alisema kuwa, “kikao hiki ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Mahakama ya Rufani wa kuhakikisha kuwa, inamaliza mashauri yote yanayosajiliwa na katika kikao hiki kuna idadi ya mashauri 50 ambapo mashauri tisa ni rufaa za madai, mashauri 11 ni rufaa za jinai, mashauri 17 ni maombi ya madai na mashauri 13 ni maombi ya jinai.”

Mhe. Wanjah alisema kwamba, maandalizi yote yamekamilika kwa maana ya ratiba ya kikao (Causelist) na hati za kuitwa shaurini zilitolewa kwa wakati.

“Ni matarajio yetu kuwa kutokana na mpango wa kusikiliza mashauri kuandaliwa mapema pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa kila jalada, kikao hiki kitafikia malengo yaliyokusudiwa,” alieleza Naibu Msajili huyo.

Kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha awali cha wadau wote wanaohusika na mashauri yanayotarajiwa kusikilizwa ambapo Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Jopo hilo, Mhe. Ferdinand Wambali aliongoza kikao hicho na kueleza kuwa, moja ya malengo ya kikao hicho cha awali ni kuangalia hali ya maandalizi ya kikao cha kusikiliza mashauri.

Aidha, kikao hicho kinafanyika sanjari na vikao vingine vinavyofanyika katika Kanda za Dar es Salaam, Mbeya, Moshi, Shinyanga na Sumbawanga ikiwa ni muendelezo wa vikao vya Mahakama ya Rufani kwa mwaka huu.           

Majaji wanaohusika na usikilizaji wa mashauri katika kikao hicho ni Jopo la Majaji wanne wa Mahakama ya Rufani ambao ni Mhe. Ferdinand Wambali (Mwenyekiti wa Jopo), Mhe. Panterine Kente, Mhe.Zainab Muruke na Mhe. Leila Mgonya.


Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wanaosikiliza mashauri katika Kikao cha Kusikiliza mashauri Kanda ya Arusha, Mhe. Ferdinand Wambali (kushoto) akilakiwa na Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha alipowasili mkoani Arusha kwa ajili ya kikao cha Mahakama hiyo.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Ferdinand Wambali akiongoza kikao cha awali cha maandalizi pamoja na wadau kabla ya kuanza kikao cha kusikiliza mashauri. Kikao hiki kilifanyika tarehe 21 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Wanjah Hamza akifafanua jambo wakati wa Kikao cha awali cha maandalizi ya usikilizaji mashauri ya Mahakama ya Rufani mkoani Arusha kilichofanyika tarehe 21 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Wajumbe mbalimbali waliohudhuria kikao cha awali cha maandalizi ya Kikao cha Mashauri cha Mahakama ya Rufani wakiwa katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 21 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni