Jumatano, 23 Oktoba 2024

JAJI MKUU AONGOZA JOPO LA MAJAJI WA RUFANI SHINYANGA –MASHAURI 43 KUSIKILIZWA

Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama - Shinyanga

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma anaongoza jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani kusikiliza mashauri ya Rufani katika Masjala ndogo ya Mahakama hiyo iliyopo Kanda ya Shinyanga. 

Mhe Prof. Juma ambaye aliwasili mkoani Shinyanga tarehe 19 Oktoba, 2024 anaongoza jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani watatu ambao tayari wameanza kusikiliza mashauri hayo kuanzia tarehe 21 Oktoba, 2024.

Katika kikao hicho, jumla ya mashauri 43 yanatarajiwa kusikilizwa kuanzia tarehe 21 Oktoba, 2024 kilipoanza kikao hicho hadi tarehe 08 Novemba, 2024 ambapo kinatarajiwa kuhitimishwa.

Kikao hicho kinatarajiwa kupunguza kiasi kikubwa cha mashauri yaliyokuwa yamekatiwa rufaa kwenye Mahakama hiyo.

Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani wanaosikiliza mashauri hayo wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania ni Mhe. Lugano Mwandambo, Mhe. Sam Rumanyika na Mhe. Amour Khamis.

Aidha, Jaji Mkuu ameambatana na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Abeesiza Kalegeya.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga alipowasili katika Mahakama hiyo yeye pamoja na Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani kusikiliza mashauri ya katika Kanda hiyo. Kulia kwa Jaji Mkuu ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali.

Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga ambapo Kikao cha Kusikiliza Mashauri ya Mahakama ya Mahakama ya Rufani kinaendelea.

(Habari hii imehaririwa MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni