Na LIGHTNESS KABAJU-Mahakama, Divisheni ya Kazi
Mahakakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, jana tarehe 25 Oktoba, 2024 imefanya kikao na kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kutathmini na kupata mrejesho wa matumizi ya mfumo mpya wa kielectroniki wa usimamizi na uendeshaji wa mashauri.
Mkutano huo ambao ulifunguliwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Salma Maghimbi ulijumuisha wadau kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Mawakili Tanganyika, Jeshi la Magereza na baadhi ya Naibu Wasajili, Mahakimu na wataalamu wa Mahakama.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Maghimbi alieleza kwamba Mahakama ya Tanzania inatekeleza kwa vitendo nguzo ya tatu ya ushirikishwaji wa wadau ili kuwa na uelewa wa pamoja katika jukumu muhimu la utoaji haki kwa wananchi.
Jaji Mfawidhi aliainisha mafanikio yaliyotokana na matumizi ya mfumo huo tangu kuanzishwa kwake tarehe 6 Novemba, 2023 kama nyenzo muhimu katika uendeshaji wa mashauri ndani ya Mahakama ya Tanzania.
Alieleza pia kuwa mfumo huo unachagiza utoaji haki kwa wakati, utunzaji bora wa nyaraka za kimahakama, upatikanaji wa nyaraka kwa haraka, kupunguza mlundikano wa mashauri, kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri na kupunguza tuhuma za mazingira ya rushwa mahakamani.
Mhe. Maghimbi alitumia nafasi hiyo kuwaasa wadau waliohudhuria kikao hicho kufanya kazi kwa uadilifu na pia kuwa tayari katika kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kutoa maoni ili kuzidi kuboresha mfumo huo.
Katika Kikao hicho, Afisa TEHAMA wa Mahakama, Bw. Tumaini Malima alipata wasaa wa kuwapitisha wadau katika mfumo huo ambapo alionesha maboresho yaliyofanyika tangu ulipoanza kutumika.
Pia alianisha matazamio ya mbele ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi zaidi katika uboreshwaji wa mfumo huo ili kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza.
Kadhalika, wadau walipata nafasi ya kutoa mrejesho wao na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya katika utoaji haki wa wakati lakini pia kwa maboresho yanayozidi kutolewa siku hadi siku ili kutoa urahisi kwa wadau na wananchi katika matumizi ya mfumo huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni