Jumapili, 27 Oktoba 2024

TEKNOLOJIA YA KUWAWEZESHA VIZIWI KUSHIRIKI KWENYE USULUHISHI YAJA

Na MAGRETH      KINABO- Mahakama

 

Mahakama ya Tanzania kupitia Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu ya Tanzania, kwa kushirikiana na Taasisi ya ESS Creative & Legal Foundation imeandaa teknolojia maalum ya kubadilisha sauti kuwa maandishi ili kuwawezesha viziwi na watu wenye usikivu hafifu kushiriki katika kutatua migogoro kwa kutumia njia ya mbadala.

 

Teknolojia hiyo iliyoanzishwa ijulikanao kwa jina la ‘Communication Access Real Time Transalation,’ lengo lake ni kukuza uelewa wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya mbadala yaani usuluhishi na upatanishi kwa watu hao.

 

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa akiwasilisha mada ya usuluhishi kwenye mafunzo maalumu ya siku moja yaliyoshirikisha watu  10 wenye tatizo hilo, Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma amesema teknolojia hiyo itasaidia kusukuma huduma ya haki mbele kwa kuwa itawafikia watu wengi.

 

“Mafunzo haya teknolojia hii ni ya kipekee na yamefungua milango kwa   watu wengine wenye tatizo hilo, ambao watakuwa na migogoro mfano ya kibiashara na mingineyo kuweza kutumia njia ya usuluhishi kwa ajili ya kuitatua, hivyo tunahitaji ushirikiano wenu,”amesema Mhe. Jaji Maruma.

 

Mhe.  Maruma amesema njia hiyo ya usuluhishi inatumika nchini na dunia nzima, haina gharama na inaokoa muda kwa kuwa inachukua siku 30 shauri kukamilika  kuliko kutumia Mahakama, ambayo kesi inaweza kutumia muda mrefu. Huku akisisitza kwamba njia hiyo ina usiri na haitumii mashahidi.

 

Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa Kituo hicho, Mhe. Angela Bahati akitoa mada ya upatanishi amesema ni mchakato wa haraka na hauna taratibu ngumu,hujenga urafiki na uhusiano, pia ulikuwa unatumiwa na mababu zetu, familia, viongozi wa dini , yakiwemo mabaraza ya kata.

 

Akifunga mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, wa Kituo hicho, Mhe. Arufani Kweka amesema amewataka watu hao, kutumia vizuri mafunzo waliyoyapata na kusaidia wengine ili wawe chachu ya kutatua migogoro kwa njia mbadala badala ya kwenda mahakamani.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya ESS Creative & Legal Foundation, Bw. Erick Mukiza, ambayo inafanya masuala ya usuluhishi amesema utaalamu huo, wa kubadilisha sauti kuwa maandishi aliupata nchini Marekani. Hivyo mafunzo hayo yametolewa chini ya ufadhili kutoka Serikali ya Marekani, huku akiongeza kwamba awali alikuwa akifahamu Lugha ya alama, ndio iliyokuwa inatumika, lakini sasa teknolojia hiyo inaweza ikatumika ili kuwezesha mawasiliano kwa watu hao.

 

“Utaalamu huu nimejifunza kutoka nchi ya Marekani, hivyo ni muhimu kwa nchi yetu ikatumia teknolojia hii ili kuwawezesha watu wenye ulemavu huo kujumuhishwa kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi. Hivyo nitashirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa teknolojia hii inawafikia watu wengi,” amesema Mukiza.

 

Amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inaonesha kwamba watu wenye ulemavu huo wako karibu ya milioni moja.

 

Ameongeza kwamba mafunzo hayo, yametolewa kwa watu hao, kutoka taasisi ya Furaha ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi Tanzania (FUWAVITA) kama mradi wa mfano na yanatajiwa kutolewa watu wenye ulemavu huo, nchini zima kwa  kushirikisha jinsia zote.

 

Naye Mkurugenzi wa FUWAVITA, Bi. Aneth Gerana Isaya, amesema wanashukuru kupata mafunzo hayo. Pia taasisi hiyo imeweza kuwafikia wanawake wajasiriamali 3,500 na wanakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo wanaomba wasaidiwe ili kuweza kuzitatua.

 

Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma akitoa mada kuhusu umuhimu wa kutumia usuluhishi katika kutatua migogoro  na teknolojia hiyo kwenye mafunzo hayo.


Teknolojia ya CART ikibadilisha sauti ya Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma kuwa maandishi kwa ajili ya kuwawezesha viziwi na watu wenye usikivu hafifu kupata elimu hiyo, itakayowasaidia kutatua migogoro kwa kutumia njia ya usuluhishi.

 

 Bi.Rahel Peter, ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo, akinukuu elimu kuhusu masuala ya usuluhishi baada ya kufuatilia kwenye screen ya TV.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taasisi ya ESS Creative & Legal Foundation, Bw. Erick Mukiza akizungumzia kuhusu teknolojia hiyo katika mafunzo hayo.

Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma(katikati), Majaji wa Kituo hicho, Mhe. Arufani Kweka (kushoto) na Mhe. Angela Bahati(kulia) wakifuatilia maelezo ya  Mkurungezi huyo kwenye screen ya TV.

 

 Jaji wa Kituo hicho, Mhe. Angela Bahati akitoa mada kuhusu uhuhimu wa  kutumia  upatanishi katika kutatumia migogoro.

Teknolojia hiyo, ikibadilisha sauti ya Jaji wa Kituo hicho, Mhe. Angela Bahati kuwa maandishi kwenye screen ya TV. 

  Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya ESS Creative & Legal Foundation, Bw. Erick Mukiza (kushoto), Mtendaji wa Kituo hicho, Bi. Hellen Mkubwa(katikati) na Naibu Msajili wa Kituo hicho, Mhe. Augustina Mmbando (kulia) wakifuatilia jambo kwenye screen hiyo.


Mshiriki wa mafunzo hayo, Bi. Victoria Phillimoni akiuliza jambo kwa kutumia Lugha ya alama.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Bi. Agnes Kikoti akiuliza jambo kwa kutumia Lugha ya alama.

 Mtaalamu wa Lugha ya Alama, Bi. Nyamasheki Malima akibadilisha  Lugha ya alama  kuwa Lugha ya saudí ili teknolojia hiyo iweze kubadilisha kuwa  maandishi  kwa ajili ya kuwezesha washiriki wa mafunzo hayo, kuelewa kinachoulizwa.

Naibu Msajili wa Kituo hicho, Mhe. Augustina Mmbando akielezea jambo kwenye mafunzo hayo.

Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma(kushoto) akimkabidhi cheti cha kushiriki mafunzo hayo Mkurugenzi wa taasisi ya Furaha ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi Tanzania (FUWAVITA), Bi. Aneth Gerana Isaya.

 Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma(kushoto) akimkabidhi cheti mshiriki wa mafunzo hayo, Bi. Leah Kyejo.

Jaji wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Arufani Kweka (kushoto)akifunga mafunzo hayo, (kulia) ni Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma.

 Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja.

Picha ya juu na chini Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo, wakiwemo watumishi wengine wa Kituo hicho.




Meza Kuu ikiwa picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo, wakiwemo watumishi wengine wa Kituo hicho, wakinyanyua mikono ikiwa ni alama ya kushangilia jambo.
 

Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma(kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa taasisi ya Furaha ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi Tanzania (FUWAVITA), Bi. Aneth Gerana Isaya.

Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma(kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi  ya ESS Creative & Legal Foundation, Bw. Erick Mukiza(kulia).



 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni