Na. RICHARD MATASHA-Mahakama, Mtwara
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, tarehe 25 Oktoba, 2024 ilifanya tafrija maalum ya kuwaaga wastaafu 16 waliostaafu katika utumishi wa umma mwaka 2023 na mwaka 2024.
Tukio hilo lilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kanda ya Mtwara na watumishi wengine. Lengo la tafrija hiyo lilikuwa kutambua mchango wa wastaafu hao katika kuimarisha mfumo wa haki na huduma za kisheria nchini.
Akizungumza katika htafrija hiyo, Jaji Mfawidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara,Mhe. Rose Ebrahim aliwapongeza wastaafu hao kwa kuitumikia jamii kwa muda mrefu.
"Mlipokuwa katika utumishi mlimsaidia mwananchi wa kawaida kupata haki yake, na mchango wenu utakumbukwa daima," alisema.
Wastaafu walipata fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za burudani, ikiwa ni pamoja na ngoma za asili na nyimbo mbalimbali. Hali hiyo ilileta furaha na kumbukumbu nzuri, huku wastaafu wakikumbushana mambo ya zamani na changamoto walizokutana nazo katika utumishi wao.
Walitumia pia nafasi hiyo kueleza jinsi walivyoweza kuvuka vikwazo na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya Mahakama.
Wakati wa kuhitimisha hafla hiyo, zawadi maalum zilitolewa kwa kila mstaafu kama ishara ya shukrani kwa huduma zao. Wastaafu walionyesha shukrani zao kwa pamoja na kuahidi kuendelea kutoa mchango katika jamii kwa njia nyingine.
Sehemu ya ukumbi ulioandaliwa kwa ajili ya hafla hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim akihutubia katika hafla hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wastaafu wanawake. Wengine katika picha ni Majaji wa Mahakama Kuu Mtwara, Mhe. Saidi Ding’ohi (wa pili kutoka kushoto), Mhe. Martha Mpaze (wa pili kutoka kulia), Naibu Msajili, Mhe. Seraphine Nsana (kulia mwisho) na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, Mhe. Consolatha Singano (kushoto mwisho).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wastaafu wanaume.
Baadhi ya wastaafu hao wakikata keki kusherehekea utumishi wao uliotukuka.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara inayojumuisha Mikoa ya Lindi na Mtwara wakifurahia katika hafla hiyo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni