• Yajipanga kupeleka huduma za Mahakama za Mwanzo tatu
Na AMANI MTINANGI, Mahakama -Tabora
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi amesema Kanda hiyo imeanza kujipanga kuinga’arisha Wilaya ya Sikonge kwa kuanza mchakato wa kufungua Mahakama za Mwanzo tatu ambazo ni Kipili, Nyahua na Kitunda.
Mhe. Dkt. Mambi alibainisha hayo hivi karibuni wakati wa ziara ya ukaguzi wa kuona maeneo muhimu yenye uhitaji mkubwa wa Mahakama kwa kuzingatia kuwa Wilaya hiyo ina Mahakama moja pekee ya Mwanzo licha ya ukubwa wa kilometa za mraba 27,873 na wakazi 353,686 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Akiwa ziarani, Jaji Mfawidhi alitembelea katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Sikonge ambapo alikutana na Mkuu wa Wilaya hiyo na kusema kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imejipanga kufanya utaratibu wa kuanzisha Mahama za mwanzo katika maeneo muhimu ya Wilaya ya Sikonge.
“Ninatambua kuwa Wilaya ya Sikonge ni kubwa kuliko baadhi ya nchi za Afrika na ina wakazi wengi, ninatambua pia kuwa ni muhimu sana kuhakikisha huduma za kimahama zinapatikana karibu na kama ilivyo kwenye Mkakati wa Mahakama na sisi tutaanzisha mchakato wa kupata Mahakama kadhaa kama ambavyo wananchi wa Sikonge wanaomba,” alisema Jaji Mfawidhi.
Akizungumza wakati wa kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Sikonge, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Cornel Lucas Magembe alisema uchache Mahakama katika Wilaya hiyo kimekuwa ni kilio cha muda mrefu cha Wilaya hiyo, hivyo wameiomba Mahakama kuongeza idadi ya Mahakama katika Wilaya hiyo kwa kuwa wananchi wanasubiria kwa hamu huduma za Mahakama na kwamba Uongozi wa Wilaya upo tayari kutoa majengo ya kuanzia katika maeneo matatu ambayo ni Kitunda, Kipili na Nyahua.
“Wananchi wa Sikonge wamekuwa na kiu ya kupata Mahakama za Mwanzo, ninaiomba Mahakama kuongeza idadi ya Mahakama, sisi kama uongozi wa Wilaya tupo tayari kutoa sehemu ya majengo Taasisi za Serikali katika Kata za Kitunda, Kipili na Nyahua na tayari maeneo ya kujenga Mahakama hizo yametengwa taratibu za kuwamilikisha zinaendelea na zipo katika hatua mbalimbali,” alieleza Mhe.Magembe.
Akitoa shukrani katika Kijiji cha Kitunda kwa niaba ya uongozi wa Mahakama, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel Munda aliwashukuru Viongozi wa Wilaya Sikonge na Kijiji cha Kitunda kwa ushirikiano wanaoendelea kuuonesha kwa Mahakama.
“Kwa niaba ya Mahakama ya Kuu Kanda ya Tabora ninawashukuru uongozi wa Wilaya Sikonge na Kijiji cha Kitunda kwa jinsi ushirikiano wenu na utayari wa kutupatia maeneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama,” alisema Bw. Munda.
Uongozi wa Kijiji cha Kitunda uliiomba Mahakama kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za Mahakama na kusema kuwa wapo tayari kupokea huduma hiyo na kuchangia nguvukazi.
“Mahakama ni chombo cha haki, tunawaomba mtusaidie kutengeneza mazingira wezeshi ya kupatikana huduma hiyo, sisi wananchi wa Kitunda tupo tayari kuchangia nguvukazi iwapo itahitajika,” alisema Mtendaji Kata wa Kitunda, Bw. Maulid Rashid Magope.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel Munda wa kwanza (aliyesimama kulia) akitoa neno la shukrani kwa Uongozi wa Kata ya Kitunda Wilaya ya Sikonge.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni