Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo tarehe 25Oktoba, 2024 aliongoza kikao cha menejimenti kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Kondoa.
Pamoja naye alikuwepo pia Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe.Sylvia Lushasi,Mtendaji wa Mahakama Dodoma, Bw. Sumera Manoti pamoja na watumishi wengine wa Dodoma na Singida ambao ni wajumbe wa kikao hicho.
Lengo la kikao hicho lilikuwa kupeana taarifa mbalimbali za kiutendaji na kiutumishi pamoja na kujua hali ya uendeshaji wa mashauri ndani ya Kanda hiyo.
Kabla ya kikao hicho kuanza, Jaji Mfawidhi na wajumbe wengine walipata elimu ya Afya ya Akili kwa ustawi binafsi na Taasisi kutoka kwa mwezeshaji ambaye ni Daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe iliyopo Dodoma, Dkt. Sarah Mwakasege.
Pamoja na mambo mengi yaliyoongelewa katika kikao hicho, Jaji Masabo aliwakumbusha Viongozi kuhusu umuhimu wa kutembelea miradi ya ujenzi wa Mahakama inayoendelea katika Kanda hiyo.
Alisema kuwa kufanya hivyo kutawafanya kujua maendeleo ya kina ya miradi hiyo na kuweza kubaini changamoto mbalimbali na kuzitolea taarifa na kuzitatua kwa wakati.
Aidha, Jaji Mfawidhi alisisitiza wajumbe wa mkutano huo kufuata miongozo na taratibu zilizopo na kuweka utaratibu wa kutembelea Mahakama za Mwanzo katika maeneo yao ya kazi ili kufahamu uhalisia wa Mahakama hizo.
“Tufuate miongozo na taratibu zilizopo, tusifanye kazi kwa mazoea, mazoea ni mabaya sana kwani ulimwengu umebadilika. Kwa hiyo, tujitahidi kufanya kazi kwa weledi na uwajibikaji na kila mmoja ajitume kama ambavyo sheria na taratibu za kazi zinavyomtaka ,” alisisitiza.
Taarifa mbalimbali za mashauri pamoja na maeneo mengine ya kiutawala ziliwasilishwa katika kikao hicho huku baadhi ya wajumbe wakipata fursa ya kuchangia na kuweka mikakati mizuri ya kazi.
Akizungumzia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Jaji Masabo alisema, “Kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Mahakama katika eno hili, tafadhali tusisuesue katika matumizi ya TEHAMA.”
Kadhalika, Jaji Mfawidhi aliwataka watumishi kujifunza na kuwa na taaluma zaidi ya moja ili kuweza kuongeza ufanisi.
Kabla ya kufunga kikao hicho, Mhe.Dkt. Masabo alitoa maelekezo kwa Mahakimu Wafawidhi ambao ni wajumbe wa kikao hicho wafanyie kazi kwenye mfumo na kuhakikisha kuwa taarifa zimehuishwa nakila shauri lina nyaraka muhimu kama ambavyo linatakiwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akisaini kitabu cha wageni katika Mahakama ya Wilaya Kondoa.
Daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe iliyopo Dodoma, Dkt. Sarah Mwakasege(aliyesimama) akitoa mada ya afya ya akili kwa wajumbe wa kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni