Na AMINA SAIDI-Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara
Katika hatua ya kuimarisha huduma za Mahakama, wajumbe kutoka Mahkama Kuu Zanzibar, Divisheni ya Biashara, wanafanya ziara ya kubadilishana uzoefu na wenzao kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania.
Ziara hiyo ya siku nne ambayo ilianza tarehe 27 Oktoba, 2024 imelenga kujifunza mifumo mbalimbali ya usimamizi wa mashauri na huduma zinazotolewa mahakamani ili kuboresha utendaji na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Katika siku ya kwanza, wajumbe walipata fursa ya kujionea mifumo mbalimbali, ikiwemo wa usajili wa wateja na kupokea mrejesho kutoka kwao. Mfumo huo uliobuniwa mahakamani hapo, unasaidia kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma za kimahakama.
Pia, walijadili umuhimu wa kuzingatia maoni ya wateja ili kuboresha huduma zinazotolewa. Kadhalika,wajumbe walipata maarifa kuhusu mfumo wa unukuzi na tafsiri.
Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar na Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Muumini Khamis Kombo, alioneshwa kushangazwa na kufurahia namna mfumo huo ulivyoweza kubadilisha sauti kuwa maneno.
“Mfumo huu ni muhimu katika kuhakikisha kuwa mashauri yanashughulikiwa kwa usahihi na kwa wakati muafaka, huku pia zikizingatiwa lugha na tamaduni tofauti za wahusika”, alisema Jaji Kombo.
Sambamba na hilo, Wajumbe walijifunza kuhusu mfumo wa usimamizi wa mashauri, ambao unarahisisha mchakato wa kusimamia mashauri ya kibiashara.
Wajumbe walionesha kufurahishwa na namna mfumo huu unavyoweza kupangia wenyewe mashauri kwa Majaji na kutoa taarifa sahihi na kwa wakati zinazosaidia katika kufanya maamuzi bora na kuongeza ufanisi wa mahakama.
Walipitishwa pia katika kanuni mbalimbali zinazohusiana na usikilizaji wa mashauri ya kibiashara, ambazo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa taratibu za kisheria zinazingatiwa. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa wahusika wanapata haki zao katika mchakato wa kisheria.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe. Joyce Minde (aliyesimama), akitoa neno la utangalizi kwa wajumbe kutoka Mahkama Kuu Zanzibar.
Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Bi Amina Said, akielezea namna mifumo mbalimbali ya kielekroniki inavyofanya kazi Mahakamani hapo.
Wajumbe wakipitishwa katika mfumo wa kusajili taarifa za wateja na kupokea maoni, katika eneo la mapokezi.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia wasilisho la mfumo wa unukuzi na tafsiri.
Mmoja kati ya wajumbe akiwa kwenye majaribio ya vifaa vya kurekodi mienendo ya mashauri.
Wajumbe wa meza kuu wakipongeza mawasilisho yaliyotolewa.Baadhi ya wajumbe wakipitia nyaraka mbalimbali katika maktaba ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni