Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 30 Oktoba, 2024 amewasili Mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe kuhudhuria Mkutano wa saba wa Mamlaka ya Kikatiba Afrika (CJCA) unaotarajia kufanyika kuanzia kesho tarehe 31 Oktoba, 2024 hadi tarehe 03 Novemba, 2024.
Mhe. Prof. Juma ataungana na Majaji na Wadau wengine wa Sekta ya Sheria kutoka nchi mbalimbali kushiriki Mkutano huo.
Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo; Utu wa binadamu kama thamani ya msingi na kanuni: Chanzo cha tafsiri ya kikatiba, ulinzi wa haki za msingi za binadamu na utekelezaji.
Aidha, katika Mkutano huo, Mhe. Prof. Juma atakuwa kwenye moja ya Paneli ya Wazungumzaji watakaozungumzia na kuongoza majadiliano kuhusu mada isemayo; Dhana ya utu wa binadamu katika sheria ya kikatiba.
Aidha, Mkutano huo utahudhuriwa pia na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine zitakazoshiriki katika Mkutano huo ni Zambia, Malawi, Msumbiji, Lesotho, Afrika Kusini, Namibia, Somalia, Sierra Leone, Togo, Uturuki, Misri, Ushelisheli, Urusi, Senegal na nyingine.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika chumba cha wageni maalum (VIP) wakati alipowasili leo tarehe 30 Oktoba, 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Victoria Falls nchini Zimbabwe kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa saba wa Mamlaka ya Kikatiba Afrika (CJCA).
(Picha na MARY GWERA, Mahakama ya Tanzania)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni