Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro
Malalamiko yanayowasilishwa na wananchi kuhusu shughuli za kimahakama yamepungua kwa kiasi kikubwa kwa mwaka 2024, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Ukaguzi wa Shughuli za Kimahakama, Mrejesho kwa Umma na Maadili, Mhe. Maira Kasonde, amesema.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye Mkutano wa kila mwezi na Vyombo na Habari, leo tarehe 31 Oktoba, 2024 uliofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro, Mhe. Kasonde amebainisha kuwa malalamiko yaliyopokelewa hadi Septemba 2024 yamepungua kwa asilimia 47.
“Malalamiko yaliyopokelewa hadi Septemba 2024 yalipungua kwa asilimia 47, ikilinganishwa na malalamiko 1,192 yaliyopokelewa mwaka 2022,” amesema alipokuwa anazungumzia mchango wa Kituo cha Huduma kwa Mteja katika upatikanaji haki kwa wakati, kuongeza imani ya Wananchi na uwajibikaji.
Amebainisha kuwa tangu Kituo cha Huduma kwa Mteja kilipoanzishwa tarehe 1 Machi, 2022, jumla ya malalamiko ambayo yamepokelewa ni 2,814. Mhe. Kasonde ameeleza kuwa kuanzia Machi hadi Desemba, 2022, malalamiko yaliyopokelewa ni 1,192.
Amewaambia Waandishi wa Habari kuwa kati ya Januari na Desemba, 2023, jumla ya malalamiko yaliyopokelewa yalipungua na kufikia 987 na kati ya Januari na Septemba, 2024 yakaporomoka hadi kufikia 635.
“Kupungua kwa malalamiko ni ishara ya wazi kwamba yamekuwa yanafanyiwa kazi na wahusika na wananchi kuridhika. Kiwango cha Wananchi kuridhika na huduma zitolewazo na Mahakama ya Tanzania kimepanda kutoka asilimia 78 mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 88 mwaka 2023,” Mhe. Kasonde amesema.
Amefafanua kuwa Kituo cha Huduma kwa Mteja kimekuwa kioo cha Mhimili wa Mahakama ambapo kupitia taarifa zake Mahakama hujitazama na kuona mapungufu ya ubora wa huduma zake na kupelekea kuchukua hatua stahiki naza haraka ili kuziboresha.
Mhe. Kasonde ameeleza pia kuwa Kituo kinasaidia kuleta uwajibikaji kwa watoa huduma (Watumishi wa Mahakama) ambao, kwa namna moja ama nyingine, mara kadhaa wamekuwa wakilalamikiwa na Wananchi.
“Baadhi ya Watumishi wa Mahakama, wakiwemo Mahakimu, tayari wamechunguzwa na kupelekwa mbele ya Vyombo vya Nidhamu kutokana na taarifa zilizopokelewa na kuchakatwa katika Kituo...
...Kituo kinasimamia makubaliano ya huduma kwa mteja yaliyowekwa na Mahakama kupitia Mkataba wa Huduma kwa Mteja, 2020 (Judiciary Client Service Charter) katika kuleta uwazi na uwajibikaji,” amesema.
Mhe. Kasonde ametumia jukwaa hilo kuwaomba Wananchi kuendelea kutumia Kituo hicho, ambacho ni miongoni mwa mifumo ya kupokea na kushughulikia mrejesho (maoni, malalamiko, pongezi na maulizo) iliopo katika Mahakama kwa kupiga Simu ya Bure (Toll Free) Namba 0800 750 247 ambayo iko hewani masaa 24 siku saba za wiki.
“Namba hii imeunganishwa katika Mfumo (Judiciary Call Center System) ambao hupokea mrejesho kwa njia ya kidigitali, unaweza kuhudumia zaidi ya wateja 30 kwa wakati mmoja na una huduma ya WhatsApp na Chatbot,” amesema.
Mhe. Kasonde amefafanua pia kuwa mfumo huo wa Kituo umeunganishwa na mifumo mama ya kielektroniki ya Mahakama, ukiwemo wa Menejimenti ya Mashauri na Sema na Mahakama ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za mteja na unahifadhi sauti za mazungumzo mahsusi kwa ajili ya kufanya rejea na ufuatiliaji wa ombi la mteja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni