Ijumaa, 1 Novemba 2024

BONANZA LA MICHEZO LA WATUMISHI WA MAHAKAMA LATIKISA MOSHI

  • Mamia ya wananchi wajitokeza viwanja vya Limpopo TPC 
  • Jaji Mfawidhi asisitiza michezo kuwa kipaumbele kwa watumishi wa Mahakama

Na PAUL PASCAL -Mahakama Moshi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Lilian Mongella amewataka watumishi wa Mahakama kuwa na utamaduni wa kukutana mara kwa mara na kufanya mazoezi na michezo ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha afya zao.

Jaji Mongella alitoa rai hiyo hivi karibuni katika uwanja wa Limpopo uliopo katika Kiwanda cha Sukari TPC Moshi wakati wa uzinduzi wa bonanza maalumu amballiliwakutanisha watumishi wote kwa lengo la kufahamiana na kukumbushana wajibu wa majukumu yao ya kila siku.

"Watumishi waliofika hapa ni wa Wilaya sita ambazo zinaunda Kanda yetu ya Moshi, yaani Mahakama za Wilaya  Moshi, Hai, Siha, Himo, Rombo, Same na Mwanga,  lengo ni kufahamiana, kukosoana, kukumbushana na kufurahi kwa kuwa michezo ni afya,” alisema.

Jaji Mfawidhi alibainisha pia kuwa bonanza hilo linafuta madaraja baina ya watumishi na Viongozi na kuweka uwanja wa kusikiliza changamoto, maoni na ushauri kutoka kwa watumishi wa vituo vyote.

Kadhalika, aliwahimiza watumishi wote kuwa na ratiba ya michezo katika vituo vyao vya kazi. Kwetu sisi wa Mahakama Kuu tunafanya mazoezi kila siku ya Jumanne na Alhamisi kuanzia saa 10.30 jionini vema wote tukaiga utamaduni huu kwa maslahi ya afya zetu,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya MoshiAdriani Kilimialiwahimiza watumishi kushirikiana katika maeneo ya kazi.

Tukitaka kufanikiwa katika kufikia malengo yetu, suala la ushirikiano ni lazima liwepo kati yetu,tutumie michezo na mazoezi kama nyenzo ya kujenga ushirikiano baina yetu,” alisema, huku akiwarejesha watumishi kwenye methali inayosema, “Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.” 

Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ilifanya bonanza la michezo kwa watumishi kwa kujumuisha jumla ya michezo 10, ikiwemo riadha mita 900 na mita 100 kwa wanaume na riadha mita 600 na mita 100 kwa wanawake.

Michezo mingine ni mashindano ya baiskeli kwa wanaume na wanawake, kukimbiza kanga, kucheza karata na bao, kukimbia na yai, kukimbia kwenye gunia, kucheza muziki, mashindano ya kula pamoja na kuvuta kamba. Washindi katika bonanza hilo walipatiwa zawadi mbalimbali kama kombe na medali.

Godlisten Mwingereza kutoka Mahakama ya Wilaya Sihaambaye ndiye mshindi wa kwanza wa riadha mita 900 Wanaume akipokea zawadi ya kombe kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Lilian Mongella.

Fatuma Mwai kutoka Mahakama ya Wilaya Romboambaye ndiye mshindi wa kwanza wa riadha mita 600 Wanawake akipokea zawadi ya kombe kutoka kwa JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Lilian Mongella.

Jaji wa Mahakama Kuu Moshi, Safina Simfukwe akimkabidhi nishani ya heshima kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Lilian Mongella kwa kutambua mchango wake muhimu wa kuunganisha watumishi wa Mahakama Kanda ya Moshi kupitia michezo.

Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Hai wakishangilia nishani ya ushindi katika kipengele cha mavazi baada ya kuibuka timu bora katika mavazi ya michezo.

Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Mwanga wakishangilia zawadi ya kombe baada ya kuibuka kuwa mabingwa katika mchezo wa kuvuta kamba baada ya kuigaragaza Mahakama Kuu Moshi pamoja na Mahakama ya Wilaya Moshi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni