Ijumaa, 1 Novemba 2024

MAHAKIMU TABORA WAJIANDAA USIKILIZAJI MASHAURI YA UCHAGUZI

Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora

Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya za Tabora wamepatiwa mafunzo maalum yanayolenga kufahamu sheria, miongozo na taratibu mbalimbali za usikilizaji wa Mashauri ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unatarajia kufanyika mwezi tarehe 27 Novemba, 2024.

Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili jana tarehe 31 Oktoba, 2024 yaliyofanyika wilayani Nzega, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi alisema kwamba, mafunzo hayo yanafuatia mafunzo ya awali yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam, lengo likiwa ni kuelimishana kuhusu sheria na taratibu mbalimbali zitakazowawezesha kusikiliza kwa uadilifu mashauri ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika maeneo yao.

“Haya ni mafunzo yenye lengo la kuelimishana sheria na taratibu mbalimbali zitakazowawezesha kusikiliza mashauri ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa mna mamlaka ya kufanya hivyo, kumbukeni mnaposikiliza mashauri ya namna hii wakati mwingine yanakuwa na misukumo na mihemko ya kisiasa, ni wajibu wenu kuamua mashauri haya bila upendeleo na kwa mujibu wa viapo vyenu,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo alisema mafunzo hayo yanafanyika kwa wakati sahihi kwakuwa kinaelekea kipindi cha kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo, aliwataka washiriki kuyatumia maarifa watakayoyapata kuongeza ufanisi katika kushughulikia migogoro ya uchaguzi.

“Tunafanya mafunzo haya wakati sahihi tunapoelekea kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni rai yangu kwenu kuyatumia maarifa mtakayoyapata muweze kuongeza ufanisi katika kushughulikia migogoro ya uchaguzi,” alisisitiza Mhe. Mazengo.

Mada walizofundishwa washiriki wa mafunzo hayo ni pamoja na Kanuni za kidemokrasia na misingi ya sheria za uchaguzi, Makosa ya kiuchaguzi, uandishi wa hukumu za mashauri ya uchaguzi, utekelezaji wa Ari za Mahakama wakati wa uchaguzi na Maadili ya Kimahakama katika usikilizaji wa mashauri ya uchaguzi. 

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi, Majaji wa Mahakama ya Tanzania kutoka Kanda mbalimbali wakiwemo Mhe. Hamidu Mwanga, Mhe. Emmanuel Kawishe na Naibu Wasajili ambao ni Mhe. Pamela Simon Mazengo, Mhe. Fadhili Mbelwa na Mhe. Sophia Massati.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Kanda hiyo na washiriki wa mafunzo ya kufahamu sheria, miongozo na taratibu mbalimbali za usikilizaji wa Mashauri ya Uchaguzi. Wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo maalum yanayolenga kuwawezesha Mahakimu Wakazi wa Kanda hiyo kufahamu sheria, miongozo na taratibu mbalimbali za usikilizaji wa Mashauri ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.


Washiriki wa Mafunzo wakiwa ukumbini wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa.

Mafunzo yakiendelea.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Simon Mazengo akiwasilisha mada wakati wa mafunzo kwa Mahakama Wakazi wa Kanda hizo kuhusu usikilizaji wa mashauri ya uchaguzi.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama )


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni