Na Innocent Kansha - Mahakama
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani leo
tarehe 28 Novemba, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Viongozi
waandamizi wa Mahakama ya nchini Uganda ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Viongozi hao wapo nchini Tanzania kwa ziara maalum ya kujifunza na kubadilishana
uzoefu wa namna Mahakama ya Tanzania inavyotekeleza miradi ya maboresho ya huduma
za utoaji haki nchini.
Akizungumza
na ujumbe huo Jaji Kiongozi Mhe. Dkt. Siyani ameuambia kuwa, kuitembelea
Mahakama ya Tanzania kwa mara ya tatu katika nyakati toufauti ni ushahidi tosha
kuwa safari ya maboresho ya utoaji huduma za haki siyo ya siku moja.
“Mahakama
zote Duniani zinakumbana na changamoto ya ucheleweshaji wa mashauri na pia
mlundikano wa mashauri mahakamani, hata sisi Mahakama ya Tanzania tumekuwa
tukikumbana na tatizo la mlundikano wa mashauri kama ninyi Uganda. Tulidhamiria
kufanya safari ya maboresho ya huduma za utoaji haki kwa wakati iliyotuletea
mageuzi makubwa ya kupambana na mlundikano wa mashauri mahakamani,” amesema
Mhe. Dkt. Siyani.
Aidha,
Jaji Kiongozi ameongeza kuwa kupitia mawasilisho mbalimbali mliyoyapata kutoka
kwa timu ya wataalum wa Mahakama ya Tanzania kuhusu safari ya maboresho ya huduma
za Mahakama yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika nchi zima na maono ya
Mahakama ya Tanzania ijayo.
“Kupitia
faida za maboresho hayo tumeweza kupambana na ucheleweshaji wa mashauri na mlundikano
wa mashauri mahakamani kwa kasi kubwa.Uzoefu unaonyesha kuwa leo unaweza kuwa
huna mlundikano wa mashauri mahakamani lakini kwa kipindi kifupi unakagua
unakuta tayari mashauri ya mlundikano yapo, hivyo mashauri mlundikano yanaishi
kama duara,” ameongeza Jaji Kiongozi.
Vilevile,
Jaji Kiongozi ameuambia ujumbe huo kuwa, kusipokuwa na mpango mkakati ama njia
madhubuti za kuzuia kutengeneza mlundikano hakika tatizo la mlundikano wa
mashauri halitaisha kuwa tatizo mahakamani. Ili kuondokana na matatizo hayo ya
ucheleweshaji na mlundikano wa mashauri ziko njia mbalimbali zinazopaswa
kutumika kama vile kutumia sheria zilizopo, miongozo, kutengeneza waraka na
kutoa matamko ya kiutawala.
“Lengo
la kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi ni jukumu letu sote licha ya
kwamba tunatumia njia na mifumo tofauti tofauti ndiyo maana ya ziara yenu ya
kikazi ya kujifunza na kubadilisha uzoefu kwa pamoja katika maeneo mbalimbali kwa
manufaa ya Taasisi zetu,” amesisitiza Mhe. Dkt. Siyani.
Jaji
Kiongozi amesema, mawasilisho yote yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili ya
ziara hiyo yalilenga kufahamu kwa kina maboresho ya Mahakama yanayofanyika ili
kujenga uelewa mpana wa utekelezaji wake, hasa kwenye eneo la usimamizi wa
mashauri unavyosaidia utoaji wa haki kwa wakati. Mathalani huwezi kutoa haki
kwa wote na kwa wakati bila kuwa na usimamizi mathubuti wa mashauri mahakamani.
Mhe.
Dkt. Siyani ameongeza kwamba, sheria za usimamizi na uendeshaji wa mashauri
zinatakiwa kubeba mambo makuu matatu mosi sheria inatakiwa kuwa na uwezo wa
kuchunguza uhalali wa shauri kuwepo mahakamani, pia sheria inatakuwa kueleza
ukomo wa muda wa shauri kushughulikiwa mahakamani ili kumpa Jaji ama Hakimu
uthibiti wa uendeshaji wa shauri husika kwa kufanya mambo hayo kunasaidia mfumo
bora wa usimamizi wa mashauri.
“Kwa
hapa Tanzania Mahakama imekuwa ikifanya jukumu la msingi la kufanya maboresho
na marekebisho ya sheria ili kuhakikisha kwamba sheria zinaendana na uhalisia
wa usimamizi na uendeshaji bora wa mashauri na wakati mwingine sheria isiposema
inaacha mwanya wa shauri kushughulikiwa kwa njia za kiutawala hasa kutoa maelekezo
kwa njia ya waraka kuondoa mtanziko,” amesema Jaji Kiongozi.
Kwa
upande wake Naibu Jaji Mkuu wa Uganda Mhe. Richard Buteera amesema ziara hiyo ya
kikazi ya kubadilishana uzoefu imekuwa ya mafanikio makubwa kwani wamejifunza
mambo mengi mazuri yatakayosaidia kuipeleka mbele Mahakama ya Uganda katika
utoaji wa haki kwa ufanisi zaidi.
“Napenda
kuishukuru Mahakama ya Tanzania kwa mapokezi mazuri na siku ya kwanza
tumepitishwa katika mawasilisho mbalimbali yaliyotujengea msingi wa kuyatambua maboresho ya
utoaji wa huduma ya haki ikiwemo miundombinu ya kisasa, mifumo ya kielektroniki ya kusimamia mashauri, utunzaji wa kumbukumbu kidijiti mambo haya yanatumika kutolea
haki,” amesema Mhe. Buteera.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani leo tarehe 28 Novemba, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Viongozi waandamizi wa Mahakama ya nchini Uganda (hawapo pichani) ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni