Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaasa wahitimu 762 wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) kuwa na maadili mema katika kazi na kuwa tayari kukabiliana
na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza ambazo jamii inategemea kuzitatua kama
wasomi katika ngazi waliyofikia.
Mhe. Prof. Juma ametoa
rai hiyo leo tarehe 29 Novemba, 2024 wilayani hapa katika Mahafali ya 24 ya
Chuo cha Mahakama Lushoto ambayo pia yamehudhuriwa na Wajumbe wa Baraza la Ugonzi
wa Chuo, Viongozi wa Mahakama na Viongozi wengine wa Serikali na Dini mbalimbali.
“Pamoja na ujuzi, maarifa
na taaluma mliyopata hapa chuoni, Chuo hiki kinasifika kwa kuwajengea wanafunzi
na wahitimu misingi bora ya kimaadili na hivyo kukifanya Chuo chetu kuwa na
maana ya kuwepo kwake. Ninawakumbusha wahitimu kuwa, ubora wenu na mafanikio
yenu baada ya kuhitimu kwa kiasi kikubwa itategemea sana maadili mema katika
utendaji wa kazi,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha
kuwa Mahafali hayo ya 24 ni kielelezo kuwa Chuo hicho kinaendeleza utamaduni
wake wa kuongeza wahitimu waliojazwa maarifa, ujuzi na taaluma itakayosaidia
nchi na kuwasaidia wao pia katika safari ndefu ya kielimu, kimaisha mbele yao
na katika kuijenga Tanzania.
Hivyo, ni imani yake kuwa
kila mhitimu wa Astashahada ya Msingi ya Sheria (Basic Technician Certificate
in Law), Astashahada ya Sheria (Technician Certificate in Law), au wa
Stashahada ya Sheria (Diploma in Law) ameiva na yuko tayari kuja katika elimu
ya juu zaidi, au katika nafasi yoyote itakayojitokeza na yuko tayari
kukabiliana na changamoto zozote na kuzitafutia ufumbuzi.
“Kila mmoja wenu atapewa
kipande cha karatasi, au Cheti, kuthibitisha umehitimu Astashahada ya Msingi ya
Sheria, Astashahada ya Sheria au wa Stashahada ya Sheria. Muda mfupi baada ya
sherehe, kila mmoja wenu atagundua kuwa umuhimu wake utapimwa sio kwa gamba au ganda,
bali ni kwa kiasi gani utatatua changamoto zitakazojitokeza ambazo jamii
inategemea mhitimu wa daraja lako anaweza kuzitatua,” amesema.
Mhe. Prof. Juma amewasihi
wahitimu hao kwenda kuipeperushe vema bendera ya Chuo na kuwa mabalozi wa kazi
hiyo kubwa na nzuri inayoendelea IJA, kwani imejijengea heshima, ikiwemo kutoa
watumishi wengi katika Mahakama kama vile Majaji, Naibu Wasajili na wengine na
wale ambao wameajiriwa kwenye ofisi na taasisi mbalimbali chini.
Naye Mwenyekiti wa Baraza
la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Levira,
akizungumza kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu kuhutubia kwenye mahafali hayo, amewaasa
wahitimu kuwa elimu waliyopata ni mwanzo wa safari nyingine ya kupata elimu ya
juu, hasa kwa kuzingatia ushindani mkubwa ulipo katika soko la ajira na
ongezeko la wasomi nchini.
“Matumaini yangu kuwa
wote mtaendelea au mmeshaanza masomo ya ngazi za juu, ni vizuri mkajua kwamba
ni wajibu wenu kuendelea kujifunza kwani soko la ajira limegubikwa na athari za
utandawazi zenye kuhitaji mbinu mpya za kuyakabili mabadiliko hayo ambayo yapo
katika utandawazi,” amesema.
Amewasihi wale
watakaoingia kwenye ajira kuwa mabolozi wazuri wa chuo hicho na wanaweza
kulifanikisha jambo hilo kwa ujipambanua katika soko la ajira na shughuli
mbalimbali watakazokuwa wanazifanya.
Naye Mkuu wa Chuo cha IJA
na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo amesema kuwa mahafali hayo
ya 24 yanajumuisha jumla ya wahitimu 762, wakiwemo wa Astashahada ya Msingi ya
Sheria 245 (134 wanawake, sawa na asilimia 55 na 111 wanaume, sawa na asilimia
45), Astashahada ya Sheria 279 (138 wa kike, sawa na asilimia 49 na 141 wa
kiume, sawa na asilimia 51) na Stashada ya Sheria 238 (105 wa kike, sawa na
asilimia 44 na 133 wa kiume, sawa na asilimia 56).
“Mpaka kufikia mahafali
ya leo (tarehe 29 Novemba, 2024) jumla ya wahitimu 8,954 wamehitimu katika Chuo,
hiki ikilinganisha na wanachuo 27,442 waliodahiliwa mpaka sasa,” amesema na
kubainisha kwa mafanikio ya vijana hao ni zao la utumishi bora wa wahadhiri pamoja
na watumishi waendeshaji ambao siku zote wamekuwa wanajituma kuhakikisha kuwa
IJA inatoa elimu bora na sio bora elimu.
Mhe. Dkt. Kihwelo amesema
pia kuwa wahitimu hao ni zao la Baraza la Uongozi wa Chuo, ambalo limekuwa
likitoa maelekezo kwa menejimenti kuboresha utoaji wa huduma katika Chuo na
maelekezo hayo yamekuwa yakifayiwa kazi.
Mkuu wa chuo ametumia fursa hiyo kuwapongeza kwa
dhati vijana hao ambao wamefikia hatua muhimu katika maisha yao ya kuhitimu
masomo yao kwa ngazi mbalimbali hapo chuoni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni