Na Innocent Kansha - Mahakama
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, Mhe. Franco Kiswaga leo
tarehe 29 Novemba, 2024 amefungua mafunzo ya namna bora ya matumizi ya Mfumo wa
Usimamizi wa Mashauri (Electronic Case Management System) ili kuwajengea uwezo
watumishi wa Mahakama hiyo.
Akizungumza
wakati wa kufungua mafunzo hayo ya siku moja yanayofanyika katika Kituo cha
Mafunzo kilichopo Kisutu jijini Dar es salaam, Mhe Kiswaga amewakumbusha watumishi
kutambua kuwa, kwa sasa shughuli zote za uendeshaji wa mashauri mahakamani
zinatumia mifumo ya kielektroniki hivyo ni vema watumishi wote kuitambua mifumo
hiyo na kuitumia ipasavyo katika majukumu yao ya kila siku.
“Niseme
tu kwamba, watumishi wenzangu Mahakama ya Tanzania ilishaingia kwenye safari ya
Mahakama Mtandao na utoaji haki kwa njia ya mtandao ndiyo sera kuu ya Mahakama
ya Tanzania ambapo sisi kama watumishi wa Mahakama hatuwezi kuliepuka hata
kidogo ni lazima tujengeane uwezo ili twende na kasi ya mabadiliko ya sera
hii,” amesisitiza Mhe. Kiswaga.
Mhe.
Kiswaga ameongeza kuwa, mafunzo ya mifumo ya ndani na ya nje ya mara kwa mara
yataendelea kutolewa kwa watumishi wote ili kuwajengea uwezo wa kuifahamu
mifumo mama inayotumika kutolea haki kwa wakati. Mifumo hiyo itasaidia kuongeza
weledi na ufanisi wa kazi ya kuwahudumia wananchi na wadau mbalimbali wanaofika
mahakamani kupata huduma za kimahakama.
“Niwaombe
washiriki wote kuwa makini na tufungue vichwa vyetu kwa ajili ya kupata yale
yote ambayo hatuyafahamu wakati wote wa mafunzo haya kwa kuwafuatilia wakufunzi
wetu, na muwe huru kushiriki mjadala pale mtakapoona kuna kitu hakijaeleweka
msisite kuuliza kwani ndiyo njia sahihi ya kujifunza kwa vitendo,” amesema Mhe.
Kiswaga.
Aidha,
Mhe. Kiswaga amesema mifumo mingi iliyoanzishwa inasomana wakati wa utendaji
kazi wake. Watumishi wote wanatakiwa kuifahamu, kuijua na kuitumia kwa maana ya
kuifanyia kazi, lakini pia kuwafundisha na watumishi wengine ambao kwa namna
moja au nyingine huwa kubahatika kushiriki mafunzo hayo.
“Kwa
hiyo tunashukuru sana wawezeshaji watakao tupatia mafunzo siku ya leo, ni
wazoefu wa muda mrefu na pengine ni sehemu ya safari ya Mahakama ya Tanzania ya
kuelekea Mahakama Mtandao nchi nzima. Mifumo hiyo wameshiriki kuiunda na pia
wanaendelea kuifanyia kazi,” ameongeza Mhe. Franco Kiswaga.
Vilevile,
Mhe. Kiswaga akasema, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam ni
maarufu na inafahamika nchi nzima, ni rai yangu kutumia umaarufu huo kuitangaza
kwa kuwa vinara wa matumizi bora ya mifumo hiyo inayotumika kutoa haki kwa
wananchi. Mahakama ya Tanzania imewekeza fedha nyingi katika kuijenga mifumo
hiyo inapaswa ifanyiwe kazi kwa lengo lililokusudiwa la kuwasaidia wananchi
kupata haki kwa haraka na kwa wakati bila kuchelewesha haki zinazotafutwa na
wadau.
“Hii
mifumo inapoanza kufanya kazi unaweza kuja na dhana ya kupata ugumu wa aina
flani kuitumia lakini mwisho wa siku yule mlaji wa mwisho ndiye anayefaidika na
kuona umuhimu wa matumizi ya aina ya mfumo uliyomuhudumia. Kwa maana dhamira ya
Mahakama ni kumlenga mteja anayepata huduma za kimahakama hivyo ndiyo yeye
anayenufaika,” amesama Naibu Msajili huyo.
Mhe.
Kiswaga akaelezea kwa uchache faida za mifumo inayotumika kutolea haki nchini mathalani
kwa sasa suala la utoaji nakala ya hukumu kwa wadaawa siyo tena tatizo wala
Mahakama haiongelei tena siku 90. Kwa upande wa Makatibu Mahususi kazi zimezidi
kupungua mteja sasa hivi anaweza kupata nakala ya hukumu mara baada ya tu ya
mwenendo wa kesi kukamilika.
Mafunzo
hayo yaliyoandaliwa na Uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili
kuwajengea uwezo Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama hiyo. Wakufunzi
waliyoendesha mafunzo hayo walikuwa ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ambaye pia
ni Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mhe. Beda Nyaki na Afisa
TEHAMA kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam, Tumaini Malima.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, Mhe. Franco Kiswaga leo tarehe 29 Novemba, 2024 amefungua mafunzo ya namna bora ya matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri (Electronic Case Management System) ili kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama hiyo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, Mhe. Franco Kiswaga akitafakari jambo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mhe. Beda Nyaki akitoa historia ya Mahakama ya Tanzania kuelekea safari ya Mahakama Mtandao.
(Picha na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni